The chat will start when you send the first message.
1Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kuondoka Misri, walifika Jangwa la Sinai siku hiyo hiyo.
2Baada ya kuondoka Refidimu, waliingia katika Jangwa la Sinai na Israeli wakapiga kambi pale jangwani mbele ya mlima.
3Kisha Musa akakwea kwenda kwa Mungu, naye Bwana akamwita kutoka ule mlima, akasema, “Hivi ndivyo utakavyosema na nyumba ya Yakobo na utakachowaambia Waisraeli:
4‘Ninyi wenyewe mmeona nililofanya huko Misri, jinsi nilivyowabeba kwenye mabawa ya tai na kuwaleta kwangu.
5Sasa, mkinitii kikamilifu na kutunza agano langu, basi ninyi mtakuwa hazina yangu ya pekee miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu,
6ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndio maneno utakayosema kwa Waisraeli.”
7Kwa hiyo Musa akarudi, akawaita wazee wa watu na kuwaambia maneno yote ambayo Bwana alikuwa amemwamuru ayaseme.
8Watu wote wakajibu kwa pamoja, “Tutafanya kila kitu Bwana alichokisema.” Naye Musa akarudisha majibu yao kwa Bwana .
9Bwana akamwambia Musa, “Nitakujia katika wingu zito, ili watu wanisikie nikinena nawe na kila mara waweke tumaini lao kwako.” Kisha Musa akamwambia Bwana yale ambayo watu walikuwa wamesema.
10Naye Bwana akamwambia Musa, “Nenda kwa watu ukawaweke wakfu leo na kesho. Waambie wafue nguo zao
11na wawe tayari siku ya tatu, kwa sababu siku hiyo, Bwana atashuka juu ya Mlima Sinai machoni pa watu wote.
12Weka mipaka kuzunguka mlima kwa ajili ya watu, uwaambie, ‘Mwe waangalifu, msije mkapanda mlimani au kuugusa. Yeyote atakayeugusa mlima atauawa.
13Hakika atapigwa mawe au kupigwa mishale; mkono wa mtu hautamgusa. Akiwa mwanadamu au mnyama, hataruhusiwa kuishi.’ Ila tu wakati baragumu itakapopigwa kwa mfululizo, ndipo watu wote watakapopanda mlimani.”
14Baada ya Musa kushuka kutoka mlimani akawaendea watu na kuwaweka wakfu, wakafua nguo zao.
15Kisha akawaambia watu, “Jitayarisheni kwa ajili ya siku ya tatu. Mwanaume yeyote asimkaribie mwanamke.”
16Asubuhi ya siku ya tatu kulikuwa na ngurumo na radi pamoja na wingu nene juu ya mlima na mlio mkubwa sana wa tarumbeta. Kila mmoja aliyekuwa kambini akatetemeka.
17Kisha Musa akawaongoza watu kutoka kambini kukutana na Mungu, nao wakasimama chini ya mlima.
18Mlima Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi, kwa sababu Bwana alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi kutoka tanuru kubwa, na mlima wote ukatetemeka kwa kishindo,
19nayo sauti ya tarumbeta ikawa kubwa zaidi na zaidi. Kisha Musa akazungumza, nayo sauti ya Mungu ikamjibu.
20Bwana akashuka juu ya Mlima Sinai na akamwita Musa apande juu mlimani. Kwa hiyo Musa akapanda juu,
21naye Bwana akamwambia Musa, “Shuka ukawaonye watu ili wasijipenyeze kutafuta kumwona Bwana , na wengi wao wakaangamia.
22Hata makuhani, watakaomkaribia Bwana ni lazima wajiweke wakfu, la sivyo Bwana atawaadhibu.”
23Musa akamwambia Bwana , “Watu hawawezi kupanda Mlima Sinai kwa sababu wewe mwenyewe ulituonya ukisema, ‘Wekeni mipaka kuuzunguka mlima na kuutenga kama patakatifu.’ ”
24Bwana akajibu, “Shuka ukamlete Haruni pamoja nawe. Lakini makuhani pamoja na watu wasije wakalazimisha kuja kwa Bwana , nisije nikawaadhibu.”
25Basi Musa akashuka kwa watu na kuwaambia lile aliloambiwa.