The chat will start when you send the first message.
1“Mtwae Haruni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
2Mshonee Haruni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima.
3Waambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Haruni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani.
4Haya ndio mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kizibau, kanzu, joho lililofumwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Haruni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
5Waambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi.
6“Tengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi.
7Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kizibau.
8Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.
9“Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli
10kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine.
11Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu,
12na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kizibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Haruni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za Bwana .
13Tengeneza vijalizo vya dhahabu
14na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.
15“Tengeneza kifuko cha kifuani kwa ajili ya kufanya maamuzi, kazi ya fundi stadi. Kitengeneze kama kile kizibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa.
16Kitakuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja na upana wa shibiri moja, na kikunjwe mara mbili.[#28:16 Shibiri moja ni sawa na sentimita 22.]
17Kisha weka safu nne za vito vya thamani juu yake. Safu ya kwanza itakuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi;
18katika safu ya pili itakuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi;
19safu ya tatu itakuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto;
20na safu ya nne itakuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Yote yatiwe kwenye vijalizo vya dhahabu.
21Patakuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kwa jina mojawapo la wana wa Israeli, kila kimoja kichorwe kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.
22“Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani, tengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba.
23Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili yake, uzifungie kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani.
24Funga ile mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete zilizo katika pembe za hicho kifuko cha kifuani,
25nazo zile ncha nyingine za mkufu zifunge kwenye vile vijalizo viwili, na uziunganishe na vile vipande vya mabega vya kile kizibau upande wa mbele.
26Tengeneza pete mbili za dhahabu, uziunganishe kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibau.
27Tengeneza pete nyingine mbili za dhahabu, na uziunganishe sehemu ya chini ya vipande vya mabega, upande wa mbele wa kile kizibau, karibu na pindo, juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kizibau.
28Pete za kifuko cha kifuani zitafungwa kwenye pete zile za kizibau kwa kamba ya buluu, ziunganishwe na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwa kile kizibau.
29“Wakati wowote Haruni anapoingia Mahali Patakatifu, atakuwa na yale majina ya wana wa Israeli moyoni mwake juu ya kile kifuko cha kifuani cha uamuzi, kama kumbukumbu ya kudumu mbele za Bwana .
30Pia weka Urimu na Thumimu ndani ya kifuko cha kifuani, yawe juu ya moyo wa Haruni kila mara aingiapo mbele za Bwana . Kwa hiyo siku zote Haruni atakuwa na uwezo kufanya maamuzi kwa ajili ya Waisraeli mbele za Bwana .[#28:30 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.]
31“Shona joho la kizibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu,
32na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike.
33Tengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga.
34Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile.
35Ni lazima Haruni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za Bwana , ili asije akafa.
36“Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa:
37Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba.
38Haruni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Haruni daima ili zikubalike kwa Bwana .
39“Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi.
40Watengenezee wana wa Haruni makoti, mishipi na kofia, ili kuwapa ukuu na heshima.
41Baada ya kumvika Haruni ndugu yako pamoja na wanawe nguo hizi, wapake mafuta na kuwabariki. Waweke wakfu ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
42“Watengenezee nguo za ndani za kitani zitakazofunika mwili, kutoka kiunoni hadi mapajani.
43Haruni na wanawe ni lazima wavae haya kila wanapoingia katika Hema la Kukutania au wanaposogelea madhabahu wakati wa kutoa huduma katika Mahali Patakatifu, ili wasije wakafanya kosa wakafa.
“Haya yawe maagizo ya kudumu kwa Haruni na vizazi vyake.