The chat will start when you send the first message.
1Kisha Bwana akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande hadi nchi niliyomwahidi Abrahamu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’
2Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
3Pandeni mwende katika nchi inayotiririka maziwa na asali. Lakini mimi sitaenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.”
4Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yoyote.
5Kwa kuwa Bwana alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ”
6Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima Horebu.
7Basi Musa alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania”. Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa Bwana , angeenda hadi Hema la Kukutania, nje ya kambi.
8Wakati wowote Musa alipoenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Musa hadi aingie kwenye Hema.
9Kila mara Musa alipoingia ndani ya Hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Bwana akizungumza na Musa.
10Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la Hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake.
11Bwana angezungumza na Musa uso kwa uso, kama vile mtu anavyozungumza na rafiki yake. Kisha Musa angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka kwenye Hema.
12Musa akamwambia Bwana , “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’
13Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.”
14Bwana akajibu, “Uso wangu utaenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.”
15Kisha Musa akamwambia, “Kama Uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa.
16Mtu yeyote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipoenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”
17Bwana akamwambia Musa, “Nitakufanyia jambo lile uliloomba, kwa sababu ninapendezwa nawe, nami ninakujua kwa jina lako.”
18Kisha Musa akasema, “Basi nioneshe utukufu wako.”
19Ndipo Bwana akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, Bwana , mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”
20Lakini Mungu akasema, “Hutaweza kuuona uso wangu, kwa kuwa hakuna mtu yeyote awezaye kuniona akaishi.”
21Kisha Bwana akasema, “Kuna mahali karibu nami ambapo unaweza kusimama juu ya mwamba.
22Utukufu wangu unapopita, nitakuweka gengeni kwenye mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hadi nitakapokuwa nimepita.
23Kisha nitaondoa mkono wangu nawe utaona mgongo wangu; lakini kamwe uso wangu hautaonekana.”