Ezekieli 30

Ezekieli 30

1Neno la Bwana likanijia kusema:

2“Mwanadamu, toa unabii na useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Ombolezeni ninyi na mseme,

“Ole wa siku ile!”

3Kwa kuwa siku ile imekaribia,

siku ya Bwana imekaribia,

siku ya mawingu,

siku ya maangamizi kwa mataifa.

4Upanga utakuja dhidi ya Misri,

nayo maumivu makuu yataijia Kushi.

Mauaji yatakapoangukia Misri,

utajiri wake utachukuliwa

na misingi yake itabomolewa.

5Kushi na Putu, Ludi na Arabia yote, Kubu na watu wa nchi ya agano watauawa kwa upanga pamoja na Misri.

6“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana :

“ ‘Wale walioungana na Misri wataanguka

na kiburi cha nguvu zake kitashindwa.

Kutoka Migdoli hadi Aswani,

watauawa ndani yake kwa upanga,

asema Bwana Mwenyezi.

7Hizo nchi zitakua ukiwa

miongoni mwa nchi zilizo ukiwa,

nayo miji yao itakuwa magofu

miongoni mwa miji iliyo magofu.

8Ndipo watajua kuwa mimi ndimi Bwana ,

nitakapoiwasha Misri moto

na wasaidizi wake wote watapondwa.

9“ ‘Siku hiyo wajumbe watatoka kwangu kwa merikebu, ili kuwatia hofu Ethiopia, wakiwa katika hali yao ya kuridhika. Maumivu makali yatawapata siku ya maangamizi ya Misri, kwa kuwa hakika itakuja.

10“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Nitakomesha makundi ya Misri

kwa mkono wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.

11Yeye na jeshi lake, taifa lililo katili

kuliko mataifa yote,

ataletwa ili kuangamiza nchi.

Watafuta panga zao dhidi ya Misri

na kuijaza nchi kwa waliouawa.

12Nitakausha vijito vya Mto Naili,

na kuiuza nchi kwa watu waovu;

kwa mkono wa wageni, nitaifanya nchi ukiwa

na kila kitu kilicho ndani yake.

Mimi Bwana nimenena haya.

13“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Nitaangamiza sanamu

na kukomesha vinyago katika Memfisi.

Hapatakuwa tena na mkuu katika nchi ya Misri,

nami nitaeneza hofu katika nchi nzima.

14Nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa[#30:14 yaani Misri ya Juu]

na kuitia moto Soani,

nami nitaipiga Thebesi kwa adhabu.

15Nitaimwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu,[#30:15 Kiebrania ni Sini]

ngome ya Misri,

nami nitakatilia mbali

makundi ya Thebesi.

16Nitaitia moto nchi ya Misri;

Pelusiumu itagaagaa kwa maumivu makuu.

Thebesi itachukuliwa na tufani,

Memfisi itakuwa katika taabu daima.

17Wanaume vijana wa Oni na wa Pi-Besethi[#30:17 yaani Heliopoli ( Mji wa Jua ); #30:17 yaani Bubasti]

wataanguka kwa upanga

nayo hiyo miji itatekwa.

18Huko Tapanesi mchana utatiwa giza

nitakapovunja nira ya Misri;

hapo kiburi cha nguvu zake kitakoma.

Atafunikwa na mawingu

na vijiji vyake vitatekwa.

19Kwa hiyo nitaipiga Misri kwa adhabu,

nao watajua kuwa Mimi ndimi Bwana .’ ”

20Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa kwanza, siku ya saba, neno la Bwana likanijia kusema:

21“Mwanadamu, nimevunja mkono wa Farao mfalme wa Misri. Haukufungwa ili upone au kuwekewa kipande cha ubao ili upate nguvu za kuweza kuchukua upanga.

22Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Mimi ni kinyume na Farao mfalme wa Misri. Nitavunja mikono yake yote miwili, ule mkono ulio mzima pia na ule uliovunjika na kuufanya upanga uanguke toka mkononi mwake.

23Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi zote.

24Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli na kuutia upanga wangu mkononi mwake, lakini nitavunja mikono ya Farao, naye atalia kwa huzuni mbele yake kama mtu aliyetiwa jeraha la kumfisha.

25Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, lakini mikono ya Farao italegea. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana , nitakapoutia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye ataunyoosha dhidi ya Misri.

26Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi nyingine. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana .”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.