The chat will start when you send the first message.
1Wakati huu Bwana akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, na Bwana akamtendea Sara kama alivyoahidi.
2Sara akapata mimba, na akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, katika majira yale Mungu alikuwa amemwahidi.
3Abrahamu akampa huyo mwana ambaye Sara alimzalia jina Isaka.[#21:3 maana yake Kicheko au Anacheka]
4Isaka alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru.
5Abrahamu alikuwa na umri wa miaka mia moja Isaka mwanawe alipozaliwa.
6Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, na kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.”
7Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Abrahamu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Lakini nimemzalia mwana katika uzee wake.”
8Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya. Siku ile Isaka aliyoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa.
9Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hajiri Mmisri alimzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki.
10Hivyo Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mjakazi huyu mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mjakazi huyo kamwe hatarithi na mwanangu Isaka.”
11Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe.
12Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana huyo na mjakazi wako. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka.
13Nitamfanya huyu mwana wa mjakazi wako kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”
14Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hajiri. Akaviweka begani mwa Hajiri, akamwondoa pamoja na kijana. Hajiri akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.
15Maji yalipokwisha kwenye kiriba, Hajiri akamwacha kijana chini ya kichaka.
16Kisha akaenda akaketi kama umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Akiwa ameketi pale, akaanza kulia kwa huzuni.
17Mungu akamsikia kijana akilia. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini, Hajiri? Usiogope, Mungu amesikia kijana akilia akiwa amelala pale.
18Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
19Ndipo Mungu akamfumbua Hajiri macho, akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.
20Mungu akawa pamoja na huyo kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde.
21Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akamtwalia mke kutoka Misri.
22Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Abrahamu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya.
23Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”
24Abrahamu akasema, “Ninaapa hivyo.”
25Ndipo Abrahamu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyangʼanya.
26Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ametenda hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”
27Hivyo Abrahamu akaleta kondoo na ngʼombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano.
28Abrahamu akatenga kondoo jike saba kutoka kwa kundi.
29Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ni nini maana ya hawa kondoo jike saba uliowatenga peke yao?”
30Abrahamu akamjibu, “Pokea hawa kondoo jike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”
31Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu hao wawili waliapiana hapo.
32Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi nchi ya Wafilisti.
33Abrahamu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Bwana , Mungu wa milele.
34Naye Abrahamu akakaa nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.