Hosea 7

Hosea 7

1kila mara nilipotaka kumponya Israeli,

dhambi za Efraimu zinafichuliwa

na maovu ya Samaria yanafunuliwa.

Wanafanya udanganyifu,

wezi huvunja nyumba,

maharamia hunyangʼanya barabarani,

2lakini hawafahamu kwamba

ninakumbuka matendo yao yote mabaya.

Dhambi zao zimewameza,

ziko mbele zangu siku zote.

3“Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao,

wakuu wao kwa uongo wao.

4Wote ni wazinzi,

wanawaka kama tanuru

ambalo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea

kuanzia kukanda unga

hadi umekwisha kuumuka.

5Katika sikukuu ya mfalme wetu

wakuu wanawaka kwa mvinyo,

naye anawaunga mkono wenye mizaha.

6Mioyo yao ni kama tanuru,

wanamwendea kwa hila.

Hasira yao inafoka moshi usiku kucha,

wakati wa asubuhi inalipuka

kama miali ya moto.

7Wote ni moto kama tanuru;

wanawaangamiza watawala wao.

Wafalme wake wote wanaanguka,

wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi.

8“Efraimu anajichanganya na mataifa;

Efraimu ni mkate ambao haukuiva.

9Wageni wananyonya nguvu zake,

lakini hafahamu hilo.

Nywele zake zina mvi hapa na pale,

lakini hana habari.

10Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yake,

lakini pamoja na haya yote

harudi kwa Bwana Mungu wake

wala kumtafuta.

11“Efraimu ni kama hua,

hudanganywa kwa urahisi na hana akili:

mara anaita Misri,

mara anageukia Ashuru.

12Watakapoenda, nitatupa wavu wangu juu yao;

nitawavuta chini waanguke kama ndege wa angani.

Nitakaposikia wakikusanyika pamoja,

nitawanasa.

13Ole wao, kwa sababu

wamepotoka kutoka kwangu!

Maangamizi ni yao

kwa sababu wameniasi!

Ninatamani kuwakomboa,

lakini wanasema uongo dhidi yangu.

14Hawanililii mimi kutoka mioyoni mwao,

bali wanaomboleza vitandani mwao.

Hukusanyika pamoja kwa ajili ya nafaka na divai mpya,

lakini hugeukia mbali nami.

15Niliwafundisha na kuwatia nguvu,

lakini wanapanga mabaya dhidi yangu.

16Hawamgeukii Yeye Aliye Juu Sana,

wako kama upinde wenye kasoro.

Viongozi wao wataanguka kwa upanga

kwa sababu ya maneno yao ya jeuri.

Kwa ajili ya hili watadhihakiwa

katika nchi ya Misri.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.