Isaya 25

Isaya 25

Sifa kwa Bwana

1Ee Bwana , wewe ni Mungu wangu,

nitakutukuza na kulisifu jina lako,

kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu

umetenda mambo ya ajabu,

mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.

2Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi,

mji wenye ngome kuwa magofu,

ngome imara ya wageni kuwa si mji tena,

wala hautajengwa tena kamwe.

3Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu,

miji ya mataifa katili itakuogopa wewe.

4Umekuwa kimbilio la watu maskini,

kimbilio la mhitaji katika taabu yake,

hifadhi wakati wa dhoruba

na kivuli wakati wa hari.

Kwa maana pumzi ya wakatili

ni kama dhoruba ipigayo ukuta

5na kama joto la jangwani.

Wewe wanyamazisha kelele ya wageni;

kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu,

ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo.

6Juu ya mlima huu Bwana wa majeshi ataandaa

karamu ya vinono kwa mataifa yote,

karamu ya mvinyo wa zamani,

nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

7Juu ya mlima huu ataharibu

sitara ihifadhiyo mataifa yote,

kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

8yeye atameza mauti milele.

Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

Bwana amesema hili.

9Katika siku ile watasema,

“Hakika huyu ndiye Mungu wetu;

tulimtumaini, naye akatuokoa.

Huyu ndiye Bwana , tuliyemtumaini;

sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.”

10Mkono wa Bwana utatulia juu ya mlima huu,

bali Moabu atakanyagwa chini

kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea.

11Watakunjua mikono yao katikati yake,

kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee.

Mungu atashusha kiburi chao

licha ya ujanja wa mikono yao.

12Atabomoa kuta ndefu za ngome yako

na kuziangusha chini,

atazishusha chini ardhini,

hadi mavumbini kabisa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.