Isaya 47

Isaya 47

Anguko la Babeli

1“Shuka uketi mavumbini,

ee Bikira Binti Babeli;

keti chini pasipo na kiti cha utawala,

ee Binti wa Wakaldayo.

Hutaitwa tena mwororo wala wa kupendeza.

2Chukua mawe ya kusagia, usage unga,

vua shela yako.

Pandisha mavazi yako, ondoa viatu vyako,

vuka vijito kwa shida.

3Uchi wako utafunuliwa

na aibu yako itaonekana.

Nitalipa kisasi;

sitamhurumia hata mmoja.”

4Mkombozi wetu: Bwana wa majeshi ndilo jina lake;

ndiye yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

5“Keti kimya, ingia gizani,

Binti wa Wakaldayo,

hutaitwa tena malkia wa falme.

6Niliwakasirikia watu wangu

na kuaibisha urithi wangu;

niliwatia mikononi mwako,

nawe hukuwaonea huruma.

Hata juu ya wazee

uliweka nira nzito sana.

7Ukasema, ‘Nitaendelea

kuwa malkia milele!’

Lakini hukutafakari mambo haya

wala hukuwaza juu ya kile kingeweza kutokea.

8“Sasa basi, sikiliza, ewe kiumbe mpenda anasa,

ukaaye mahali pako pa salama,

na kujiambia mwenyewe,

‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.

Kamwe sitakuwa mjane,

wala sitafiwa na watoto.’

9Haya mawili yatakupata, kufumba na kufumbua,

katika siku moja:

kufiwa na watoto, na ujane.

Yote yatakupata kwa kipimo kikamilifu,

ijapokuwa uchawi wako ni mwingi,

na uaguzi wako ni mwingi.

10Umeutegemea uovu wako,

nawe umesema, ‘Hakuna yeyote anionaye.’

Hekima yako na maarifa yako vinakupoteza

unapojiambia mwenyewe,

‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.’

11Maafa yatakujia,

nawe hutaweza kuyaondoa kwa uaguzi.

Janga litakuangukia,

wala hutaweza kulikinga kwa fidia;

msiba mkuu usioweza kuutabiri

utakujia ghafula.

12“Endelea basi na uaguzi wako,

na wingi wa uchawi wako,

ambao umeutumikia tangu utoto wako.

Labda utafanikiwa,

labda unaweza ukasababisha hofu kuu.

13Ushauri wote uliopokea umekuchosha bure!

Wanajimu wako na waje mbele,

wale watazama nyota watabiriao mwezi baada ya mwezi,

wao na wawaokoe na lile linalokuja juu yenu.

14Hakika wako kama mabua makavu;

moto utawateketeza.

Hawawezi hata kujiokoa wao wenyewe

kutokana na nguvu za mwali wa moto.

Hapa hakuna makaa ya kumtia mtu yeyote joto;

hapa hakuna moto wa kuota.

15Hayo ndiyo yote wanayoweza kuwatendea ninyi,

hawa ambao umetaabika nao

na kufanya nao biashara tangu utoto.

Kila mmoja atatoroka;

hakuna yeyote awezaye kukuokoa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.