Isaya 50

Isaya 50

Dhambi ya Israeli na utii wa mtumishi

1Hili ndilo asemalo Bwana :

“Iko wapi hati ya talaka ya mama yako

ambayo kwayo niliachana naye?

Au nimewauza ninyi kwa nani

miongoni mwa watu wanaonidai?

Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa,

kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa.

2Nilipokuja, kwa nini hapakuwa hata mtu mmoja?

Nilipoita, kwa nini hapakuwa hata mtu mmoja wa kujibu?

Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa?

Je, mimi sina nguvu za kukuokoa?

Kwa kukemea tu naikausha bahari,

naigeuza mito ya maji kuwa jangwa;

samaki wake wanaoza kwa kukosa maji

na kufa kwa ajili ya kiu.

3Ninalivika anga weusi na kufanya gunia

kuwa kifuniko chake.”

4Bwana Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa,

ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka.

Huniamsha asubuhi kwa asubuhi,

huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.

5Bwana Mwenyezi amezibua masikio yangu,

nami sikuwa mwasi,

wala sikurudi nyuma.

6Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao,

mashavu yangu wale wangʼoao ndevu zangu;

sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha

na kutemewa mate.

7Kwa sababu Bwana Mwenyezi ananisaidia,

sitatahayarika.

Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume,

nami ninajua sitaaibika.

8Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu.

Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu?

Tukabiliane uso kwa uso!

Mshtaki wangu ni nani?

Ni nani aliye mshtaki wangu?

9Ni Bwana Mwenyezi anisaidiaye mimi.

Ni nani huyo atakayenihukumu?

Wote watachakaa kama vazi,

nondo watawala wawamalize.

10Ni nani miongoni mwenu amchaye Bwana ,

na kulitii neno la mtumishi wake?

Yeye atembeaye gizani,

yeye asiye na nuru,

na alitumainie jina la Bwana ,

na amtegemee Mungu wake.

11Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto,

na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi,

nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu

na ya mienge mliyoiwasha.

Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu:

Mtalala chini kwa mateso makali.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.