The chat will start when you send the first message.
1“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki
na mnaomtafuta Bwana :
Tazameni mwamba ambako mlichongwa,
na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;
2mwangalieni Abrahamu, baba yenu,
na Sara, ambaye aliwazaa.
Wakati nilimwita alikuwa mmoja tu,
nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.
3Hakika Bwana ataifariji Sayuni,
naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote;
atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni,
nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya Bwana .
Shangwe na furaha zitakuwa ndani yake,
shukrani na sauti za kuimba.
4“Nisikilizeni, watu wangu;
nisikieni, taifa langu:
Sheria itatoka kwangu;
haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.
5Haki yangu inakaribia mbio,
wokovu wangu unakuja,
nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.
Visiwa vitanitegemea
na kungojea mkono wangu kwa matumaini.
6Inueni macho yenu mbinguni,
mkaitazame dunia chini;
mbingu zitatoweka kama moshi,
dunia itachakaa kama vazi,
na wakazi wake kufa kama inzi.
Bali wokovu wangu utadumu milele,
haki yangu haitakoma kamwe.
7“Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa,
ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu:
Msiogope mashutumu ya wanadamu
wala msitiwe hofu na matukano yao.
8Kwa maana nondo atawala kama vazi,
nao funza atawatafuna kama sufu.
Lakini haki yangu itadumu milele,
wokovu wangu kwa vizazi vyote.”
9Amka, Amka! Jivike nguvu,
ewe mkono wa Bwana ,
Amka, kama siku zilizopita,
kama vile vizazi vya zamani.
Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande,
uliyemchoma huyo mnyama mkubwa?
10Si ni wewe uliyekausha bahari,
maji ya kilindi kikuu,
uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari
ili waliokombolewa wapate kuvuka?
11Wale waliolipiwa fidia na Bwana watarudi.
Wataingia Sayuni wakiimba;
furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.
Furaha na shangwe zitawapata,
huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.
12“Mimi, naam mimi,
ndimi niwafarijie ninyi.
Ninyi ni nani hata kuwaogopa
wanadamu wanaokufa,
wanadamu ambao ni majani tu,
13kwamba mnamsahau Bwana Muumba wenu,
aliyezitanda mbingu
na kuiweka misingi ya dunia,
kwamba mnaishi katika hofu siku zote
kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu,
ambaye nia yake ni kuangamiza?
Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?
14Wafungwa waliojikunyata kwa hofu
watawekwa huru karibuni;
hawatafia kwenye gereza lao,
wala hawatakosa chakula.
15Kwa maana Mimi ndimi Bwana , Mungu wako,
ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume:
Bwana wa majeshi ndilo jina lake.
16Nimeweka maneno yangu kinywani mwako
na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu:
Mimi niliyeweka mbingu mahali pake,
niliyeweka misingi ya dunia,
niwaambiaye Sayuni,
‘Ninyi ni watu wangu.’ ”
17Amka, amka!
Simama, ee Yerusalemu,
wewe uliyekunywa kutoka mkono wa Bwana
kikombe cha ghadhabu yake,
wewe uliyekunywa hata machujo yake,
kikombe kile cha kunywea
kiwafanyacho watu kuyumbayumba.
18Kati ya wana wote aliowazaa
hapakuwa na hata mmoja wa kumwongoza;
kati ya wana wote aliowalea
hapakuwa hata mmoja wa kumshika mkono.
19Majanga haya mawili yamekuja juu yako:
ni nani awezaye kukufariji?
Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga:
ni nani awezaye kukutuliza?
20Wana wako wamezimia,
wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara,
kama swala aliyenaswa kwenye wavu.
Wamejazwa na ghadhabu ya Bwana
na makaripio ya Mungu wako.
21Kwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa,
uliyelewa, lakini si kwa mvinyo.
22Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi wako,
Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake:
“Tazama, nimeondoa mkononi mwako
kikombe kilichokufanya uyumbayumbe;
kutoka kikombe hicho,
kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu,
kamwe hutakunywa tena.
23Nitakiweka mikononi mwa watesi wako,
wale waliokuambia,
‘Anguka kifudifudi
ili tuweze kutembea juu yako.’
Ukaufanya mgongo wako kama ardhi,
kama njia yao ya kupita.”