Isaya 56

Isaya 56

Wokovu kwa wengine

1Hili ndilo asemalo Bwana :

“Dumisheni haki

na mkatende lile lililo sawa,

kwa maana wokovu wangu u karibu

na haki yangu itafunuliwa upesi.

2Amebarikiwa mtu yule atendaye hili,

mtu yule alishikaye kwa uthabiti,

yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi,

auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.”

3Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme,

“Hakika Bwana atanitenga na watu wake.”

Usimwache towashi yeyote alalamike akisema,

“Mimi ni mti mkavu tu.”

4Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana :

“Kwa matowashi washikao Sabato zangu,

ambao huchagua kile kinachonipendeza

na kulishika sana agano langu:

5hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake

kumbukumbu na jina bora

kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:

nitawapa jina lidumulo milele,

ambalo halitakatiliwa mbali.

6Wageni wanaoambatana na Bwana

ili kumtumikia,

kulipenda jina la Bwana ,

na kumwabudu yeye,

wote washikao Sabato bila kuinajisi

na ambao hushika sana agano langu:

7hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu

na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.

Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao

zitakubalika juu ya madhabahu yangu;

kwa maana nyumba yangu itaitwa

nyumba ya sala kwa mataifa yote.”

8Bwana Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye

Waisraeli waliohamishwa:

“Bado nitawakusanya wengine kwao

zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.”

Mashtaka ya Mungu dhidi ya waovu

9Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni,

njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni!

10Walinzi wa Israeli ni vipofu,

wote wamepungukiwa na maarifa;

wote ni mbwa walio bubu,

hawawezi kubweka;

hulala na kuota ndoto,

hupenda kulala.

11Ni mbwa wenye tamaa kubwa,

kamwe hawatosheki.

Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu;

wote wamegeukia njia yao wenyewe,

kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.

12Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo!

Tunywe kileo sana!

Kesho itakuwa kama leo,

au hata bora zaidi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.