Isaya 6

Isaya 6

Agizo kwa Isaya

1Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi kwenye kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu.

2Juu yake walikuwa maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka.

3Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu

ni Bwana wa majeshi;

dunia yote imejaa utukufu wake.”

4Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.

5Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi kati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.”

6Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni.

7Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”

8Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayeenda kwa ajili yetu?”

Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”

9Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa:

“ ‘Mtaendelea daima kusikiliza,

lakini kamwe hamtaelewa;

mtaendelea daima kutazama,

lakini kamwe hamtatambua.’

10Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu,

fanya masikio yao yasisikie,

na upofushe macho yao.

Wasije wakaona kwa macho yao,

na wakasikiliza kwa masikio yao,

wakaelewa kwa mioyo yao,

nao wakageuka, wakaponywa.”

11Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?”

Naye akanijibu:

“Hadi miji iwe imeachwa magofu

na bila wakazi,

hadi nyumba zitakapobaki bila watu,

na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa,

12hadi Bwana atakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana,

na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa.

13Hata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi,

itaharibiwa tena.

Lakini kama vile mvinje au mwaloni

ubakizavyo visiki unapokatwa,

ndivyo mbegu takatifu

itakavyokuwa kisiki katika nchi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.