The chat will start when you send the first message.
1Baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli wakamuuliza Bwana , “Ni nani atakayetangulia apande mbele yetu kutupigania dhidi ya Wakanaani?”
2Bwana akajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia; nimewapa hiyo nchi mikononi mwao.”
3Ndipo wanaume wa Yuda wakawaambia Wasimeoni ndugu zao, “Pandeni pamoja nasi katika nchi tuliyopewa, ili tupate kupigana na Wakanaani. Sisi pia tutaenda pamoja nanyi katika sehemu yenu mliyopewa.” Basi Wasimeoni wakaenda pamoja nao.
4Yuda aliposhambulia, Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, nao wakawaua watu elfu kumi huko Bezeki.
5Huko ndiko walipomkuta huyo Adoni-Bezeki, nao wakapigana naye na kuwafukuza Wakanaani na Waperizi.
6Adoni-Bezeki pia alikimbia, nao wakamfuata na kumkamata, wakamkata vidole vyake gumba vya mikono na vya miguu.
7Ndipo Adoni-Bezeki akasema, “Wafalme sabini waliokuwa wamekatwa vidole vyao vya gumba vya mikono na vya miguu walikuwa wakiokota makombo chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa haya kwa yale niliyowatendea.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko.
8Wanaume wa Yuda wakashambulia pia Yerusalemu na kuiteka. Wakaupiga mji kwa upanga na kuuchoma kwa moto.
9Baada ya hayo, watu wa Yuda wakateremka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, na Negebu, na nchi ya Shefela.[#1:9 au upande wa magharibi chini ya vilima]
10Yuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (mji huu hapo awali uliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai.
11Kutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (mji huu hapo awali uliitwa Kiriath-Seferi).
12Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayepigana dhidi ya Kiriath-Seferi na kuuteka.”
13Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda; kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa, akaolewa naye.
14Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”
15Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
16Wazao wa yule Mkeni, baba mkwe wa Musa, wakapanda pamoja na watu wa Yuda kutoka Mji wa Mitende, wakaenda kuishi miongoni mwa watu wa jangwa la Yuda huko Negebu karibu na mji wa Aradi.[#1:16 yaani Yeriko]
17Basi wanaume wa Yuda wakaenda na Wasimeoni ndugu zao, wakawashambulia Wakanaani walioishi Sefathi, nao wakauangamiza huo mji kabisa. Kwa hiyo huo mji ukaitwa Horma.[#1:17 maana yake Maangamizi]
18Watu wa Yuda wakatwaa pia Gaza, Ashkeloni na Ekroni, kila mji na vijiji vyake vinavyouzunguka.
19Bwana alikuwa pamoja na watu wa Yuda. Wakaimiliki nchi ya vilima, lakini hawakuweza kuwafukuza watu waliokaa katika hiyo tambarare, kwa sababu walikuwa na magari ya vita ya chuma.
20Kama vile Musa alivyoahidi, Kalebu alipewa Hebroni, naye akawafukuza wana watatu wa Anaki.
21Hata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, walioishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini.
22Basi nyumba ya Yusufu wakashambulia Betheli, naye Bwana alikuwa pamoja nao.
23Walipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo awali uliitwa Luzu),
24wale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuoneshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.”
25Hivyo akawaonesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote.
26Yule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambalo ndilo jina lake hadi leo.
27Lakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na makazi yake, au watu wa Taanaki na makazi yake, au watu wa Dori na makazi yake, au watu wa Ibleamu na makazi yake, au watu wa Megido na makazi yake, kwa kuwa Wakanaani walikuwa wameamua kuishi katika nchi ile.
28Israeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa.
29Wala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi miongoni mwao.
30Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, na walioishi Nahaloli, bali Wakanaani hao walibaki miongoni mwao; lakini waliwatia katika kazi ya kulazimishwa.
31Wala Asheri hawakuwafukuza wale walioishi huko Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeki wala Rehobu,
32na kwa sababu ya jambo hili Waasheri wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi.
33Wala Naftali hawakuwafukuza wale walioishi Beth-Shemeshi wala wale walioishi Beth-Anathi; lakini Naftali nao pia wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi, nao wale walioishi Beth-Shemeshi na Beth-Anathi wakawa watumishi wao katika kazi ya kulazimishwa.
34Waamori wakawazuilia Wadani kwenye nchi ya vilima, na hawakuwaacha washuke kuingia kwenye sehemu tambarare.
35Waamori pia walikuwa wameamua kuendelea kuishi katika Mlima Heresi, Aiyaloni na Shaalbimu; lakini nguvu ya nyumba ya Yusufu ilipoongezeka, wao pia wakashindwa na wakalazimika kuingia katika kazi ya kulazimishwa.
36Mpaka wa Waamori ulikuwa kuanzia Genge la Akrabimu, kuendelea hadi Sela na kuelekea juu.