Waamuzi 10

Waamuzi 10

Tola

1Baada ya Abimeleki, Tola mwana wa Pua mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, aliyeishi huko Shamiri, katika nchi ya vilima ya Efraimu, akainuka kuokoa Israeli.

2Akawa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na tatu. Ndipo akafa, naye akazikwa huko Shamiri.

Yairi

3Baada yake akafuatiwa na Yairi, Mgileadi, aliyekuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na mbili.

4Alikuwa na wana thelathini waliopanda punda thelathini. Nao walikuwa na miji thelathini huko Gileadi, inayoitwa Hawoth-Yairi hadi leo.

5Yairi akafa, naye akazikwa huko Kamoni.

Yefta

6Tena Waisraeli wakatenda maovu machoni pa Bwana . Wakaabudu Mabaali na Maashtorethi, na miungu ya Aramu, miungu ya Sidoni, miungu ya Moabu, miungu ya Waamoni, na miungu ya Wafilisti. Na kwa kuwa Waisraeli walimwacha Bwana wala hawakuendelea kumtumikia,

7hivyo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Waisraeli. Naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni,

8ambao waliowaonea na kuwatesa mwaka huo. Kwa miaka kumi na nane wakawatesa Waisraeli wote upande wa mashariki mwa Mto Yordani huko Gileadi, katika nchi ya Waamori.

9Waamoni nao wakavuka Yordani ili kupigana na Yuda, Benyamini na nyumba ya Efraimu, nayo nyumba ya Israeli ikawa katika taabu kubwa.

10Ndipo Waisraeli wakamlilia Bwana wakasema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, kumwacha Mungu wetu na kutumikia Mabaali.”

11Bwana akawaambia, “Wamisri, Waamori, Waamoni, Wafilisti,

12Wasidoni, Waamaleki na Wamaoni walipowadhulumu ninyi, nanyi mkanililia na kuomba msaada, je, sikuwaokoa mikononi mwao?

13Lakini ninyi mmeniacha na kuitumikia miungu mingine, kwa hiyo sitawaokoa tena.

14Nendeni mkaililie ile miungu mlioichagua. Hiyo miungu na iwaokoe mnapokuwa katika taabu!”

15Lakini Waisraeli wakamwambia Bwana , “Tumetenda dhambi. Ututendee lile unaloona kuwa jema kwako, lakini twakusihi utuokoe sasa.”

16Nao wakaiondoa hiyo miungu migeni kati yao nao wakamtumikia Bwana . Naye akahuzunika kwa sababu ya taabu ya Israeli.

17Waamoni walipoitwa vitani na kupiga kambi kule Gileadi, Waisraeli walikusanyika na kupiga kambi huko Mispa.

18Viongozi wa watu wa Gileadi wakaambiana wao kwa wao, “Yeyote atakayeanzisha mashambulizi dhidi ya Waamoni atakuwa kiongozi wa wote wanaoishi Gileadi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.