The chat will start when you send the first message.
1Palikuwa na mtu aliyeitwa Mika kutoka nchi ya vilima ya Efraimu.
2Akamwambia mama yake, “Zile shekeli elfu moja na mia moja za fedha zilizochukuliwa kwako, ambazo nilisikia ukizinenea maneno ya laana, hizi hapa; mimi ndiye niliyezichukua.”[#17:2 Shekeli 1,100 ni sawa na kilo 13.]
Ndipo mama yake akamwambia, “Bwana na akubariki, mwanangu.”
3Alipozirudisha zile shekeli elfu moja na mia moja za fedha kwa mama yake, mama yake akamwambia, “Mimi nimeiweka fedha hii wakfu kwa Bwana ili mwanangu atengeneze sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu. Mimi nitakurudishia wewe.”
4Hivyo akamrudishia mama yake ile fedha, naye mama yake akachukua shekeli mia mbili za hiyo fedha na kumpa mfua fedha, ambaye aliifanyiza kinyago na sanamu. Navyo vikawekwa ndani ya nyumba ya Mika.[#17:4 Shekeli 200 za fedha ni sawa na kilo 2.3 za fedha.]
5Basi Mika alikuwa na mahali pa ibada za sanamu. Akatengeneza kizibau, pamoja na miungu ya nyumbani, na kumweka mmoja wa wanawe kuwa kuhani wake.
6Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme; kila mtu alifanya alivyoona ni vyema machoni pake.
7Palikuwa na kijana Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, aliyekuwa akiishi miongoni mwa watu wa kabila la Yuda.
8Huyu kijana akatoka mji huo wa Bethlehemu ya Yuda na kutafuta mahali pengine pa kuishi. Alipokuwa akisafiri, akafika nyumbani kwa Mika katika nchi ya vilima ya Efraimu.
9Mika akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?”
Akamjibu, “Mimi ni Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, ninatafuta mahali pa kuishi.”
10Ndipo Mika akamwambia, “Ishi pamoja nami, uwe baba yangu na kuhani wangu, nami nitakupa shekeli kumi za fedha kila mwaka, pamoja na nguo na chakula.”[#17:10 Shekeli 10 za fedha ni sawa na gramu 115 za fedha.]
11Hivyo yule Mlawi akakubali kuishi pamoja na Mika, naye akawa kama mmoja wa wanawe.
12Basi Mika akamweka wakfu huyo kijana Mlawi, naye huyo akawa kuhani wake na kuishi nyumbani mwake.
13Mika akasema, “Sasa najua Bwana atanitendea mema, kwa kuwa Mlawi huyu amekuwa kuhani wangu.”