The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana :
2“Hili ndilo asemalo Bwana , Mungu wa Israeli: ‘Andika katika kitabu maneno yote niliyonena na wewe.
3Siku zinakuja,’ asema Bwana , ‘nitakapowaleta watu wangu Israeli na Yuda kutoka uhamishoni, na kuwarudisha katika nchi niliyowapa baba zao ili kuimiliki,’ asema Bwana .”
4Haya ndio maneno aliyoyanena Bwana kuhusu Israeli na Yuda:
5“Hili ndilo asemalo Bwana :
“ ‘Vilio vya woga vinasikika:
hofu kuu, wala si amani.
6Ulizeni na mkaone:
Je, mwanaume aweza kuzaa watoto?
Kwa nini basi ninaona kila mwanaume mwenye nguvu
ameweka mikono yake tumboni
kama mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa,
kila uso ukigeuka rangi kabisa?
7Ole! Kwa kuwa siku ile itakuwa ya kutisha.
Hakutakuwa na nyingine kama hiyo.
Utakuwa wakati wa dhiki kwa Yakobo,
lakini ataokolewa kutoka dhiki hiyo.
8“ ‘Katika siku ile,’ asema Bwana wa majeshi,
‘nitaivunja nira kutoka shingoni mwao
na kuvipasua vifungo vyao;
wageni hawatawafanya tena watumwa.
9Badala yake, watamtumikia Bwana Mungu wao
na Daudi mfalme wao,
nitakayemwinua kwa ajili yao.
10“ ‘Hivyo usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,
usifadhaike, ee Israeli,’
asema Bwana .
‘Hakika, nitakuokoa kutoka mbali,
wazao wako kutoka nchi ya uhamisho wao.
Yakobo atakuwa tena na amani na usalama,
wala hakuna atakayemtia hofu.
11Mimi niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,’
asema Bwana .
‘Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote
nilikokuwa nimewatawanya,
sitawaangamiza ninyi kabisa.
Nitawaadhibu, lakini kwa haki.
Sitawaacha kabisa bila adhabu.’
12“Hili ndilo asemalo Bwana :
“ ‘Kidonda chako hakina dawa,
jeraha lako haliponyeki.
13Hakuna yeyote wa kukutetea katika shauri lako,
hakuna dawa ya kidonda chako,
wewe hutapona.
14Wale walioungana nawe wote wamekusahau,
hawajali chochote kukuhusu wewe.
Nimekupiga vile adui angekupiga,
na kukuadhibu vile mtu mkatili angekuadhibu,
kwa sababu hatia yako ni kubwa mno,
na dhambi zako ni nyingi sana.
15Kwa nini unalia kwa ajili ya jeraha lako,
yale maumivu yako yasiyoponyeka?
Kwa sababu ya uovu wako mkubwa na dhambi zako nyingi
nimekufanyia mambo haya.
16“ ‘Lakini watu wote wakuangamizao wataangamizwa;
adui zako wote wataenda uhamishoni.
Wale wote wakutekao nyara watatekwa nyara;
wote wakufanyao mateka nitawafanya mateka.
17Lakini nitakurudishia afya yako
na kuyaponya majeraha yako,’
asema Bwana ,
‘kwa sababu umeitwa mwenye kutupwa,
Sayuni ambaye hakuna yeyote anayekujali.’
18“Hili ndilo asemalo Bwana :
“ ‘Nitarudisha baraka za mahema ya Yakobo,
na kuhurumia maskani zake.
Mji utajengwa tena juu ya magofu yake,
nalo jumba la kifalme litasimama mahali pake halisi.
19Nyimbo za kushukuru zitatoka kwao
na sauti ya furaha.
Nitaiongeza idadi yao
wala hawatapungua,
nitawapa heshima
na hawatadharauliwa.
20Watoto wao watakuwa kama walivyokuwa
siku za zamani,
nayo jumuiya yao itaimarishwa mbele yangu;
nitawaadhibu wote wanaowadhulumu.
21Mmoja wao atakuwa kiongozi wao;
mtawala wao atainuka miongoni mwao.
Nitamleta karibu nami,
naye atanikaribia mimi,
kwa maana ni nani yule atakayejitolea
kuwa karibu nami?’
asema Bwana .
22‘Kwa hiyo ninyi mtakuwa watu wangu,
nami nitakuwa Mungu wenu.’ ”
23Tazama, tufani ya Bwana
italipuka kwa ghadhabu,
upepo wa kisulisuli uendao kasi
utashuka juu ya vichwa vya waovu.
24Hasira kali ya Bwana haitarudi nyuma
hadi atakapotimiza makusudi yote ya moyo wake.
Siku zijazo
mtayaelewa haya.