Yeremia 31

Yeremia 31

Mahamisho kurudi kwa shangwe

1“Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu,” asema Bwana .

2Hili ndilo asemalo Bwana :

“Watu watakaopona upanga

watapata upendeleo jangwani;

nitakuja niwape Israeli pumziko.”

3Bwana alitutokea zamani, akisema:

“Nimekupenda kwa upendo wa milele,

nimekuvuta kwa wema.

4Nitakujenga tena, nawe utajengeka upya,

ewe Bikira Israeli.

Utachukua tena matari yako

na kwenda kucheza na wanaofurahi.

5Utapanda tena shamba la mizabibu

juu ya vilima vya Samaria,

wakulima watapanda

na kufurahia matunda yake.

6Siku inakuja ambapo walinzi watapiga kelele

juu ya vilima vya Efraimu, wakisema,

‘Njooni, twendeni juu Sayuni,

kwake Bwana Mungu wetu.’ ”

7Hili ndilo asemalo Bwana :

“Mwimbieni Yakobo kwa furaha,

mshangilieni aliye mkuu wa mataifa.

Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme,

‘Ee Bwana , okoa watu wako,

mabaki ya Israeli.’

8Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini

na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia.

Miongoni mwao watakuwa vipofu na viwete,

mama wajawazito na wenye uchungu wa kuzaa.

Umati mkubwa wa watu watarudi.

9Watakuja wakilia;

wataomba wakati ninawarudisha.

Nitawaongoza kando ya vijito vya maji,

katika njia iliyonyooka hawatajikwaa,

kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli,

naye Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.

10“Sikieni neno la Bwana , enyi mataifa,

litangazeni katika nchi za pwani ya mbali:

‘Yeye aliyewatawanya Israeli atawakusanya

na atalichunga kundi lake la kondoo kama mchungaji.’

11Bwana atamlipia fidia Yakobo

na kuwakomboa mkononi mwa walio na nguvu kuliko wao.

12Watakuja na kupiga kelele kwa furaha katika miinuko ya Sayuni;

watashangilia ukarimu wa Bwana :

nafaka, divai mpya na mafuta,

wana-kondoo wachanga

na ndama wa makundi ya ngʼombe nitakaowapa.

Watakuwa kama bustani iliyoneshewa vizuri,

wala hawatahuzunika tena.

13Kisha wanawali watacheza na kufurahi,

vijana wa kiume na wazee pia.

Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,

nitawapa faraja na furaha badala ya huzuni.

14Nitawashibisha makuhani kwa wingi,

nao watu wangu watajazwa kwa ukarimu wangu,”

asema Bwana .

15Hili ndilo asemalo Bwana :

“Sauti imesikika huko Rama,

maombolezo na kilio kikubwa,

Raheli akiwalilia watoto wake

na anakataa kufarijiwa,

kwa sababu watoto wake hawako tena.”

16Hili ndilo asemalo Bwana :

“Izuie sauti yako kulia,

na macho yako yasitoe machozi,

kwa kuwa kazi yako itapata thawabu,”

asema Bwana .

“Watarudi kutoka nchi ya adui.

17Kwa hiyo kuna tumaini kwa siku zijazo,”

asema Bwana .

“Watoto wako watarudi nchi yao yenyewe.

18“Hakika nimeyasikia maombolezo ya Efraimu:

‘Ulinirudi kama ndama mkaidi,

nami nimekubali kutii.

Unirudishe, nami nitarudi,

kwa sababu wewe ndiwe Bwana Mungu wangu.

19Baada ya kupotea, nilitubu;

baada ya kuelewa, nilijipiga kifua.

Niliaibika na kuona haya

kwa sababu niliibeba aibu ya ujana wangu.’

20Je, Efraimu si mwanangu mpendwa,

mtoto ninayependezwa naye?

Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake,

bado ninamkumbuka.

Kwa hiyo moyo wangu unamwonea shauku,

nina huruma kubwa kwa ajili yake,”

asema Bwana .

21“Weka alama za barabara,

weka vibao vya kuelekeza.

Zingatia vyema njia kuu,

barabara ile unayoipita.

Rudi, ee Bikira Israeli,

rudi kwenye miji yako.

22Utatangatanga hata lini,

ee binti usiye mwaminifu?

Bwana ameumba kitu kipya duniani:

mwanamke atamlinda mwanaume.”

23Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo, “Nitakapowarudisha toka nchi ya kutekwa kwenu, watu walio katika nchi ya Yuda na miji yake kwa mara nyingine tena watatumia maneno haya: ‘Bwana akubariki, ee makao ya haki, ee mlima mtakatifu.’

24Watu wataishi pamoja katika Yuda na miji yake yote, wakulima na wote wanaohamahama na mifugo yao.

25Nitawaburudisha waliochoka na kuwatuliza walio na huzuni.”

26Kwa jambo hili niliamka na kuangalia pande zote. Usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.

27Bwana asema, “Siku zinakuja, nitakapoongeza idadi ya watu, na kuzidisha hesabu ya mifugo katika nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.

28Kama vile nilivyowaangalia ili kungʼoa na kubomoa, kuharibu, kuangamiza na kuleta maafa juu yao, vivyo hivyo nitawaangalia ili kujenga na kupanda,” asema Bwana .

29“Katika siku hizo, watu hawatasema tena,

“ ‘Baba wamekula zabibu chachu,

nayo meno ya watoto yakatiwa ganzi.’

30Badala yake, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe; yeyote alaye zabibu chachu, meno yake mwenyewe yatatiwa ganzi.

31“Siku zinakuja,” asema Bwana ,

“nitakapofanya agano jipya

na nyumba ya Israeli

na nyumba ya Yuda.

32Halitafanana na agano

nililofanya na baba zao

wakati nilipowashika mkono

kuwaongoza watoke Misri,

kwa sababu walivunja agano langu,

ijapokuwa nilikuwa mume kwao,”

asema Bwana .

33“Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

baada ya siku zile,” asema Bwana .

“Nitaweka sheria yangu katika nia zao,

na kuiandika mioyoni mwao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

34Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

wala mtu kumfundisha ndugu yake, akisema,

‘Mjue Bwana Mungu,’

kwa sababu wote watanijua mimi,

kuanzia aliye mdogo hata aliye mkubwa kuliko wote,” asema Bwana .

“Nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”

35Hili ndilo asemalo Bwana ,

yeye aliyefanya jua

liwake mchana,

yeye anayeamuru mwezi na nyota

kungʼaa usiku,

yeye anayeichafua bahari

ili mawimbi yake yangurume;

Bwana wa majeshi ndilo jina lake:

36“Ikiwa amri hizi zitaondoka machoni pangu,”

asema Bwana ,

“ndipo wazao wa Israeli watakoma

kuwa taifa mbele yangu daima.”

37Hili ndilo asemalo Bwana :

“Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika

na misingi ya dunia chini

ikaweza kuchunguzwa,

ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli

kwa sababu ya yote waliyoyatenda,”

asema Bwana .

38“Siku zinakuja,” asema Bwana , “mji huu utakapojengwa upya kwa ajili yangu, kuanzia mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni.

39Kamba ya kupimia itaanzia hapo kuendelea hadi kwenye kilima cha Garebu, na kisha kugeuka kuelekea Goa,

40wanakotupa maiti na majivu, na maeneo yote kuanzia Bonde la Kidroni upande wa mashariki hadi pembe ya Lango la Farasi patakuwa mahali patakatifu kwa Bwana . Mji huu kamwe hautangʼolewa wala kubomolewa tena.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.