Yeremia 8

Yeremia 8

Dhambi na uasi wa Yuda

1“ ‘Wakati huo, asema Bwana , mifupa ya wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, na mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka makaburi yao.

2Itawekwa wazi kwa jua, na mwezi, na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia, na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama kinyesi juu ya ardhi.

3Popote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asema Bwana wa majeshi.’

Dhambi na adhabu

4“Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana :

“ ‘Je, watu wanapoanguka hawainuki?

Je, mtu anapopotea harudi?

5Kwa nini basi watu hawa waliasi?

Kwa nini Yerusalemu wanaasi kila mara?

Wanangʼangʼania udanganyifu

na wanakataa kurudi.

6Nimewasikiliza kwa makini,

lakini hawataki kusema lililo sawa.

Hakuna anayetubu makosa yake

akisema, “Nimefanya nini?”

Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe

kama farasi anayeenda vitani.

7Hata korongo aliye angani

anayajua majira yake yaliyoamriwa,

nao njiwa, mbayuwayu na koikoi

hufuata majira yao ya kurudi.

Lakini watu wangu hawajui

Bwana anachotaka kwao.

8“ ‘Mwawezaje kusema, “Sisi tuna busara

kwa sababu tunayo sheria ya Bwana ,”

wakati kwa hakika kalamu ya uongo ya waandishi

imeandika kwa udanganyifu?

9Wenye hekima wataaibika,

watafadhaika na kunaswa.

Kwa kuwa wamelikataa neno la Bwana ,

hiyo hekima waliyo nayo ni ya namna gani?

10Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao,

na mashamba yao kwa wamiliki wengine.

Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,

wote wana tamaa ya kupata zaidi;

manabii na makuhani wanafanana,

wote wanafanya udanganyifu.

11Wanafunga majeraha ya watu wangu

bila uangalifu.

Wanasema, “Amani, amani,”

wakati hakuna amani.

12Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno?

Hapana, hawana haya hata kidogo,

hawajui hata kuona aibu.

Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,

watashushwa chini watakapoadhibiwa,

asema Bwana .

13“ ‘Nitayaondoa mavuno yao,

asema Bwana .

Hapatakuwa zabibu kwenye mzabibu.

Hapatakuwa na tini kwenye mtini,

na majani yake yatanyauka.

Kile nilichowapa

watanyangʼanywa.’ ”

14Kwa nini tunaketi hapa?

Kusanyikeni pamoja!

Tukimbilie kwenye miji yenye ngome,

tukaangamie huko!

Kwa kuwa Bwana Mungu wetu

ametuhukumu kuangamia,

na kutupatia maji yenye sumu tunywe,

kwa sababu tumemtenda dhambi.

15Tulitegemea amani,

lakini hakuna jema lililokuja,

tulitegemea wakati wa kupona,

lakini kulikuwa hofu tu.

16Mkoromo wa farasi wa adui

umesikika kuanzia Dani,

kwa mlio wa madume yao ya farasi,

nchi yote inatetemeka.

Wamekuja kuangamiza nchi na vyote vilivyomo,

mji na wote wanaoishi ndani yake.

17“Tazama, nitatuma nyoka wenye sumu kali kati yenu,

fira ambao hawawezi kulogwa,

nao watawauma,”

asema Bwana .

18Ee Mfariji wangu katika huzuni,

moyo wangu umezimia ndani yangu.

19Sikia kilio cha watu wangu

kutoka nchi ya mbali:

“Je, Bwana hayuko Sayuni?

Je, Mfalme wake hayuko tena huko?”

“Kwa nini wamenikasirisha kwa vinyago vyao,

kwa sanamu zao za kigeni zisizofaa?”

20“Mavuno yamepita,

kiangazi kimekwisha,

nasi hatujaokolewa.”

21Kwa kuwa watu wangu wamepondwa, nami nimepondeka pia;

ninaomboleza, nayo hofu kuu imenishika.

22Je, hakuna zeri ya kuponya katika Gileadi?

Je, hakuna tabibu huko?

Kwa nini basi hakuna uponyaji

wa majeraha ya watu wangu?

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.