Yohana 10

Yohana 10

Mchungaji mwema

1“Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyangʼanyi.

2Yeye anayeingia kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo.

3Mlinzi humfungulia lango, na kondoo huisikia sauti yake. Yeye huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi.

4Baada ya kuwatoa wote nje, yeye hutangulia mbele yao na kondoo humfuata, kwa kuwa wanaijua sauti yake.

5Lakini kondoo hawatamfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.”

6Yesu alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia.

7Kwa hiyo Yesu akasema nao tena, akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo.

8Wote walionitangulia ni wezi na wanyangʼanyi, nao kondoo hawakuwasikia.

9Mimi ndimi lango. Yeyote anayeingia zizini kupitia kwangu ataokoka. Ataingia na kutoka, naye atapata malisho.

10Mwizi huja ili aibe, aue na aangamize. Mimi nimekuja ili wapate uzima, kisha wawe nao tele.

11“Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

12Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Anapomwona mbwa-mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa-mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya.

13Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.

14“Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu, nao kondoo wangu wananijua.

15Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, ndivyo nami ninautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.

16Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili. Inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu; hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.

17Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena.

18Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu, na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”

19Waliposikia maneno haya, Wayahudi wakagawanyika.

20Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”

21Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”

Yesu akataliwa na Wayahudi

22Ikafika Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu huko Yerusalemu. Ilikuwa majira ya baridi.[#10:22 yaani Hanukkah kwa Kiebrania]

23Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika Ukumbi wa Sulemani.

24Wayahudi wakamkusanyikia, wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka hadi lini? Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie waziwazi.”[#10:24 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]

25Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia.

26Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu.

27Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata.

28Nami ninawapa uzima wa milele; hawataangamia kamwe, wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu.

29Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote, na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake.

30Mimi na Baba yangu tu umoja.”

31Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo,

32lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni kwa ipi kati ya hiyo miujiza mnataka kunipiga mawe?”

33Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Ingawa wewe ni mwanadamu, unajifanya kuwa Mungu.”

34Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Sheria yenu kwamba, ‘Nimesema kuwa ninyi ni “miungu”’?[#10:34 Za 82:6]

35Kama aliwaita ‘miungu’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka,

36je, mwawezaje kusema kwamba yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru, kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu’?

37Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini.

38Lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ni ndani yake.”

39Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao.

40Yesu akaenda tena ngʼambo ya Yordani hadi mahali Yohana alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko.

41Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yohana hakufanya muujiza wowote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.”

42Nao watu wengi wakamwamini Yesu huko.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.