Yohana 9

Yohana 9

Yesu amponya mtu aliyezaliwa kipofu

1Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa.

2Wanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi; ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”

3Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake.

4Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi.

5Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

6Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule kipofu machoni.

7Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni Kutumwa). Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.

8Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?”

9Wengine wakasema, “Ndiye.”

Wengine wakasema, “Siye, bali anafanana naye.”

Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.”

10Wakamuuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?”

11Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia, ‘Nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu,’ ndipo nikanawa nami nikapata kuona!”

12Wale wakamuuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?”

Akawajibu, “Sijui.”

Mafarisayo wachunguza kuponywa kwa kipofu

13Wakamleta yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali kwa Mafarisayo.

14Basi siku hiyo Yesu alitengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato.

15Mafarisayo nao wakaanza kumuuliza yule mtu alivyopata kuona. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”

16Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.”

Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.

17Hivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho. Wasemaje kuhusu mtu huyo?”

Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.”

18Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu akapata kuona, hadi walipowaita wazazi wake.

19Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?”

20Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu.

21Lakini hatujui jinsi anavyoweza kuona sasa, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni; yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.”

22Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi, kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Yesu kuwa ndiye Kristo atafukuzwa kutoka sinagogi.[#9:22 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]

23Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.”

24Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.”

25Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.”

26Wakamuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?”

27Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?”

28Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake! Sisi ni wanafunzi wa Musa.

29Tunajua kwamba Mungu alisema na Musa, lakini mtu huyu hatujui anakotoka.”

30Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu!

31Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii.

32Tangu zamani hatujasikia kwamba mtu amemponya yeyote aliyezaliwa kipofu.

33Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lolote.”

34Wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje.

Upofu wa kiroho

35Yesu aliposikia kuwa wamemfukuza atoke nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta, akamuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”

36Yule mtu akamjibu, “Yeye ni nani, Bwana? Niambie ili nipate kumwamini.”

37Yesu akamjibu, “Umekwisha kumwona; naye anayezungumza nawe, ndiye.”

38Yule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu.

39Yesu akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona wawe vipofu.”

40Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?”

41Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.