The chat will start when you send the first message.
1Lakini Yona alichukizwa sana akakasirika.
2Akamwomba Bwana , “Ee Bwana , hili si lile nililolisema nilipokuwa ningali nyumbani? Hii ndiyo sababu niliharakisha kukimbilia Tarshishi. Nikifahamu kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na huruma, si mwepesi wa hasira na umejaa upendo, ni Mungu ambaye hughairi katika kupeleka maafa.
3Sasa, Ee Bwana , niondolee uhai wangu, kwa kuwa ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
4Lakini Bwana akamjibu, “Je unayo haki yoyote kukasirika?”
5Yona akatoka nje akaketi mahali upande wa mashariki wa mji. Hapo akajitengenezea kibanda, akaketi kwenye kivuli chake na kungojea ni nini kitakachotokea katika mji.
6Ndipo Bwana Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu.
7Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka.
8Jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona hadi akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
9Lakini Mungu alimwambia Yona, “Je, unayo haki kukasirika kuhusu mzabibu huo?”
Akasema, “Ndiyo, ninayo haki. Nimekasirika kiasi cha kufa.”
10Lakini Bwana akamwambia, “Wewe unakasirika kwa ajili ya mzabibu huu, nawe hukuusababisha kuota wala kuutunza. Uliota usiku mmoja, nao ukafa usiku mmoja.
11Lakini Ninawi ina zaidi ya watu elfu mia moja na ishirini ambao hawawezi kupambanua kulia au kushoto, pamoja na ngʼombe wengi. Je, hainipasi kufikiri kuhusu mji ule mkubwa?”