The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa,
2“Waambie Waisraeli: ‘Mwanamke ambaye atapata mimba na kuzaa mtoto wa kiume atakuwa najisi kwa siku saba, kama anavyokuwa najisi wakati wa siku zake za hedhi.
3Naye huyo mtoto atatahiriwa siku ya nane.
4Kisha ni lazima huyo mwanamke asubiri kwa siku thelathini na tatu, ndipo atakaswe kutoka damu kwake. Hataruhusiwa kugusa kitu chochote kilicho kitakatifu au kuingia mahali patakatifu, hadi siku za kutakaswa kwake zimetimia.
5Kama alimzaa mtoto wa kike, mwanamke huyo atakuwa najisi kwa majuma mawili, kama wakati wake wa hedhi. Kisha atasubiri kwa siku sitini na sita, ndipo atatakaswa kutoka damu kwake.
6“ ‘Siku zake za utakaso kwa ajili ya mwana au binti zitakapotimia, mwanamke huyo atamletea kuhani kwenye ingilio la Hema la Kukutania mwana-kondoo mwenye umri wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, na kinda la njiwa au hua kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
7Atavitoa mbele za Bwana ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na kisha atatakasika kutokana na kutokwa na damu.
“ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya mwanamke atakayezaa mtoto wa kiume au wa kike.
8Kama huyo mwanamke hana uwezo wa kumpata mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda wawili wa njiwa, mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na mwingine kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kwa njia hii, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.’ ”