The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa,
2“Sema na Haruni na wanawe, pamoja na Waisraeli wote, uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana aliloagiza:
3Mwisraeli yeyote atakayetoa dhabihu ya ngʼombe, mwana-kondoo au mbuzi ndani ya kambi au nje yake,
4badala ya kuileta kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili kuileta kama sadaka kwa Bwana mbele ya Maskani ya Bwana , mtu huyo atahesabiwa kuwa na hatia ya kumwaga damu; amemwaga damu, na ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
5Hii ni ili Waisraeli wamletee Bwana dhabihu wanazozifanya sasa mahali pa wazi mashambani. Ni lazima wazilete kwa makuhani, yaani kwa Bwana , katika ingilio la Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu kuwa sadaka za amani.
6Kuhani atanyunyiza damu kwenye madhabahu ya Bwana katika ingilio la Hema la Kukutania, na kuyateketeza mafuta ya hiyo dhabihu kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Bwana .
7Kamwe wasitoe tena dhabihu zao kwa sanamu za mbuzi ambazo wamekuwa wakijifanyia nazo ukahaba. Hili litakuwa agizo la kudumu kwao na kwa vizazi vijavyo.’
8“Waambie: ‘Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote anayeishi miongoni mwao atakayetoa sadaka ya kuteketezwa au dhabihu
9bila kuileta kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili kutoa dhabihu kwa Bwana , mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
10“ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwao ambaye atakula damu yoyote, nitakuwa kinyume chake, na nitamkatilia mbali na watu wake.
11Kwa kuwa uhai wa kiumbe uko ndani ya damu, nami nimewapa hiyo damu ili mfanyie upatanisho kwa ajili yenu wenyewe juu ya madhabahu; damu ndiyo ifanyayo upatanisho kwa ajili ya maisha ya mtu.
12Kwa hiyo, ninawaambia Waisraeli, “Hakuna hata mmoja wenu anayeruhusiwa kula damu, wala mgeni anayeishi miongoni mwenu haruhusiwi kula damu.”
13“ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye atamwinda mnyama au ndege anayeruhusiwa kuliwa ni lazima aimwage damu na kuifunika kwa udongo,
14kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni damu yake. Ndiyo sababu nimewaambia Waisraeli, “Kamwe msile damu ya kiumbe chochote, kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni damu yake; yeyote atakayekula damu lazima akatiliwe mbali.”
15“ ‘Mtu yeyote, awe mzawa au mgeni, ambaye atakula mzoga wa kitu chochote ama kilichouawa na wanyama mwitu ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni; kisha atakuwa ametakaswa.
16Lakini kama hakufua nguo zake na kuoga, atakuwa na hatia kwa kosa hilo.’ ”