Walawi 4

Walawi 4

Sadaka ya dhambi

1Bwana akamwambia Musa,

2“Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote afanyapo dhambi bila kukusudia na akatenda lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana :

3“ ‘Ikiwa kuhani aliyepakwa mafuta amefanya dhambi na kuwaletea watu hatia, lazima alete kwa Bwana fahali mchanga asiye na dosari, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya dhambi aliyotenda.

4Atamkabidhi huyo fahali kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Bwana . Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo fahali na kumchinja mbele za Bwana .

5Kisha kuhani huyo aliyepakwa mafuta atachukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuileta katika Hema la Kukutania.

6Atachovya kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza sehemu yake mara saba mbele za Bwana , mbele ya pazia la mahali patakatifu.

7Kisha kuhani atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri iliyo mbele za Bwana katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ya huyo fahali ataimwaga chini ya hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka kwenye ingilio la Hema la Kukutania.

8Atayaondoa mafuta yote ya fahali huyo wa sadaka ya dhambi: mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani au zile zinazounganika nazo,

9figo zote mbili na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo zote,

10kama vile mafuta yanavyoondolewa kutoka kwa ngʼombe aliyetolewa sadaka ya amani. Kisha kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.

11Lakini ngozi ya huyo fahali na nyama zake zote, pamoja na kichwa na miguu yake, sehemu za ndani na matumbo,

12yaani sehemu nyingine zote zilizobaki za huyo fahali, lazima azitoe nje ya kambi hadi mahali palipo safi, ambapo majivu hutupwa; naye atamchoma kwa moto wa kuni juu ya lundo la majivu.

13“ ‘Ikiwa jumuiya yote ya Israeli watatenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana , hata kama jumuiya hawafahamu jambo hilo, wana hatia.

14Wanapotambua dhambi waliyoitenda, lazima kusanyiko walete fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi, na kuikabidhi mbele ya Hema la Kukutania.

15Wazee wa jumuiya wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali mbele za Bwana , naye huyo fahali atachinjwa mbele za Bwana .

16Kisha kuhani aliyepakwa mafuta ataingiza sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya Hema la Kukutania.

17Atachovya kidole chake kwenye damu na kuinyunyiza mara saba mbele za Bwana mbele ya hilo pazia.

18Atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu yaliyo mbele za Bwana katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu ya kuteketezea sadaka, penye ingilio la Hema la Kukutania.

19Atayaondoa mafuta yote ya yule fahali na kuyateketeza juu ya madhabahu,

20naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa.

21Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya.

22“ ‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya Bwana Mungu wake, ana hatia.

23Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete beberu asiye na dosari kuwa sadaka yake.

24Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za Bwana . Hii ni sadaka ya dhambi.

25Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu.

26Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa.

27“ ‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia, na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana , yeye ana hatia.

28Atakapofahamishwa dhambi aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kuwa sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda.

29Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka.

30Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu.

31Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Bwana . Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.

32“ ‘Akileta mwana-kondoo kuwa sadaka yake ya dhambi, atamleta jike asiye na dosari.

33Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo mwana-kondoo na kumchinja kwa ajili ya sadaka ya dhambi mahali ambako sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa.

34Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia juu ya pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na ile damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu.

35Ataondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kutoka kwa mwana-kondoo wa sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu juu ya zile sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.