The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua, na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa.
2Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo kama hicho walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote?
3La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo.
4Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu: mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote walioishi Yerusalemu?
5Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”
6Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja.
7Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’
8“Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uuache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea.
9Nao ukizaa matunda mwaka ujao, vyema! La sivyo, uukate.’ ”
10Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato.
11Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na nane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima.
12Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.”
13Yesu alipomwekea mikono yake, akasimama wima mara moja, akaanza kumtukuza Mungu.
14Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia umati ule wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”
15Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato?
16Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti ya Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na nane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”
17Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.
18Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini?
19Umefanana na punje ya haradali ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti, nao ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”
20Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha ufalme wa Mungu na nini?
21Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga hadi wote ukaumuka.”
22Yesu akapita katika miji na vijiji, akifundisha wakati alisafiri kwenda Yerusalemu.
23Mtu mmoja akamuuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?”
Yesu akawaambia,
24“Jitahidini sana kuingia kupitia mlango mwembamba, kwa maana nawaambia wengi watajaribu kuingia, lakini hawataweza.
25Mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkibisha mlango na kusema, ‘Bwana! Tufungulie mlango!’
“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako.’
26“Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’
27“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
28“Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapowaona Abrahamu, Isaka, Yakobo na manabii wote wakiwa katika ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje.
29Watu watatoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika ufalme wa Mungu.
30Tazama, kuna walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”
31Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”
32Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’
33Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa: kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.
34“Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!
35Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena hadi wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.’”[#13:35 Za 118:26]