The chat will start when you send the first message.
1Ndipo baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjia Yesu kutoka Yerusalemu na kumuuliza,
2“Mbona wanafunzi wako wanakiuka mapokeo ya wazee? Kwa maana wao hawanawi mikono yao kabla ya kula!”
3Yesu akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?
4Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’[#15:4 Kut 20:12; Kum 5:16; #15:4 Kut 21:17; Law 20:9]
5Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’
6basi hana tena sababu ya kumheshimu baba yake nacho. Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu.
7Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba:
8“ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
9Huniabudu bure;
nayo mafundisho yao
ni maagizo ya wanadamu tu.’”
10Yesu akaita umati wa watu waliokuwa hapo, akawaambia, “Sikilizeni na mwelewe:
11kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”
12Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”
13Akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu wa mbinguni hakuupanda utangʼolewa.
14Waacheni; wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”
15Petro akasema, “Tueleze maana ya huu mfano.”
16Yesu akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu?
17Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu?
18Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi.
19Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio.
20Haya ndio yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
21Yesu aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni.
22Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”
23Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”
24Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”
25Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”
26Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
27Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwa meza za bwana zao.”
28Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.
29Yesu akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko.
30Umati mkubwa wa watu wakamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya.
31Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.
32Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga watu wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.”
33Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kulisha umati mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”
34Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”
35Yesu akaagiza watu wote waketi chini.
36Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akamshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu.
37Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.
38Idadi ya watu walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.
39Baada ya kuaga umati wa watu, Yesu aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani.[#15:39 yaani Magdala katika Galilaya]