The chat will start when you send the first message.
1“Kwa maana ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu.
2Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinari moja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu.[#20:2 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja.]
3“Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi.
4Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa chochote kilicho haki yenu.’
5Hivyo basi wakaenda.
“Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo.
6Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’
7“Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna yeyote aliyetuajiri.’
“Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’
8“Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’
9“Wale vibarua walioajiriwa saa kumi na moja wakaja, na kila mmoja wao akapokea dinari moja.
10Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja.
11Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba,
12wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’
13“Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja?
14Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe.
15Je, sina haki ya kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’
16“Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
17Basi Yesu alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwaita kando wale wanafunzi kumi na wawili na kuwaambia,
18“Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Nao watamhukumu kifo
19na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!”
20Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani.
21Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika ufalme wako.”
22Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?”
Wakajibu, “Tunaweza.”
23Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”
24Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili.
25Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao.
26Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,
27naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu:
28kama vile Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
29Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu wakamfuata.
30Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapaza sauti wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
31Umati wa watu wakawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”
32Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
33Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”
34Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.