The chat will start when you send the first message.
1Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia,
2“Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi.
3Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.
4“Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’
5“Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake.
6Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua.
7Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.
8“Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja.
9Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’
10Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.
11“Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi.
12Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.
13“Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’
14“Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”
15Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake.
16Wakatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode kwake. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonesha upendeleo.
17Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”
18Lakini Yesu alifahamu kusudi lao mbaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega?
19Nionesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari.
20Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
21Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
22Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.
23Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema,
24“Mwalimu, Musa alisema, ‘Mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’
25Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane.
26Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba.
27Hatimaye, yule mwanamke naye akafa.
28Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”
29Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu.
30Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.
31Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba,
32‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”[#22:32 Kut 3:6]
33Wale umati wa watu waliposikia hayo, walishangaa sana kwa mafundisho yake.
34Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja.
35Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema,
36“Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”
37Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’[#22:37 Kum 6:5]
38Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.
39Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’[#22:39 Law 19:18]
40Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”
41Mafarisayo wakiwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza,
42“Mnaonaje kuhusu Kristo? Yeye ni mwana wa nani?”[#22:42 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]
Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”
43Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,
44“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.”’
45Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?”
46Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.