The chat will start when you send the first message.
1Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Yudea, akisema,
2“Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
3Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema:
“Sauti ya mtu aliaye nyikani,
‘Itengenezeni njia kwa ajili ya Bwana,
yanyoosheni mapito yake.’”
4Basi Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.
5Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Yudea yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani.
6Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.
7Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?
8Basi zaeni matunda yastahiliyo toba.
9Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka kwa mawe haya.
10Hata sasa shoka limeshawekwa tayari katika shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.
11“Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.[#3:11 au katika Roho Mtakatifu]
12Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”
13Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya hadi Mto Yordani ili Yohana ambatize.
14Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”
15Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.
16Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake.
17Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa; ninapendezwa sana naye.”