Mithali 16

Mithali 16

1Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu,

bali jibu la ulimi hutoka kwa Bwana .

2Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe,

bali makusudi hupimwa na Bwana .

3Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo,

nayo mipango yako itafanikiwa.

4Bwana hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe;

hata waovu kwa siku ya maangamizi.

5Bwana huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo.

Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa.

6Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa;

kwa kumcha Bwana mtu hujiepusha na ubaya.

7Njia za mtu zinapompendeza Bwana ,

huwafanya hata adui zake waishi naye kwa amani.

8Afadhali kitu kidogo pamoja na haki

kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.

9Moyo wa mtu huifikiri njia yake,

bali Bwana huelekeza hatua zake.

10Midomo ya mfalme huzungumza kwa hekima ya kiungu,

wala kinywa chake hakipotoshi haki.

11Vipimo na mizani za halali hutoka kwa Bwana ;

mawe yote ya kupimia yaliyo katika mfuko ameyafanya yeye.

12Wafalme huchukia sana kutenda maovu,

kwa maana kiti cha ufalme hufanywa imara kupitia haki.

13Wafalme hufurahia midomo ya uaminifu;

humthamini mtu asemaye kweli.

14Ghadhabu ya mfalme ni mjumbe wa mauti,

bali mtu mwenye hekima ataituliza.

15Uso wa mfalme ungʼaapo, inamaanisha uhai;

upendeleo wake ni kama wingu la mvua wakati wa vuli.

16Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu,

kuchagua ufahamu kuliko fedha!

17Njia kuu ya wanyofu huepuka ubaya;

yeye aichungaye njia yake, huchunga maisha yake.

18Kiburi hutangulia maangamizi,

roho ya majivuno hutangulia maanguko.

19Ni afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu

miongoni mwa walioteswa

kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.

20Yeyote anayekubali mafundisho hustawi,

tena amebarikiwa yeye anayemtumaini Bwana .

21Wenye hekima moyoni huitwa wenye ufahamu,

na maneno ya kupendeza huchochea mafundisho.

22Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwa wale walio nao,

bali upumbavu huleta adhabu kwa wapumbavu.

23Moyo wa mtu mwenye hekima huongoza kinywa chake,

na midomo yake huchochea mafundisho.

24Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali,

ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.

25Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu,

bali mwisho wake huelekeza mautini.

26Shauku ya mfanyakazi humhimiza kufanya kazi;

njaa yake humsukuma aendelee.

27Mtu mbaya kabisa hupanga mabaya,

maneno yake ni kama moto uunguzao.

28Mtu mpotovu huchochea ugomvi,

nayo maongezi ya upuzi huwatenganisha rafiki wa karibu.

29Mtu mkali humvuta jirani yake

na kumwongoza katika mapito yale mabaya.

30Yeye akonyezaye kwa jicho lake anapanga upotovu;

naye akazaye midomo yake amenuia mabaya.

31Mvi ni taji la utukufu;

hupatikana kwa maisha ya uadilifu.

32Ni afadhali mtu mstahimilivu kuliko shujaa,

mtu anayeitawala hasira yake kuliko yule autekaye mji.

33Kura hupigwa kwa siri,

lakini kila uamuzi wake hutoka kwa Bwana .

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.