Mithali 22

Mithali 22

1Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi;

kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.

2Tajiri na maskini wanafanana kwa hili:

Bwana ni Muumba wao wote.

3Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,

bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara.

4Unyenyekevu na kumcha Bwana

huleta utajiri, heshima na uzima.

5Katika mapito ya waovu kuna miiba na mitego,

bali yeye ailindaye nafsi yake hukaa mbali nayo.

6Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,

naye hataiacha hata akiwa mzee.

7Matajiri huwatawala maskini

naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye.

8Yeye aupandaye uovu huvuna taabu,

nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa.

9Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa

kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.

10Mfukuze mwenye dhihaka,

na mvutano utatoweka;

ugomvi na matukano vitakoma.

11Yeye apendaye moyo safi na yeye ambaye maneno yake ni ya neema,

mfalme atakuwa rafiki yake.

12Macho ya Bwana hulinda maarifa,

bali huyapinga maneno ya asiye mwaminifu.

13Mvivu husema, “Yuko simba nje!”

au, “Nitauawa katika mitaa!”

14Kinywa cha mwanamke kahaba ni shimo refu;

yeye aliye chini ya ghadhabu ya Bwana

atatumbukia ndani yake.

15Upumbavu umefungwa ndani ya moyo wa mtoto,

bali fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali naye.

16Yeye anayemdhulumu maskini ili kujiongezea mali,

naye anayempa tajiri zawadi, wote huwa maskini.

Misemo thelathini ya wenye hekima

17Tega sikio na usikie misemo ya wenye hekima,

elekeza moyo wako kwenye yale nifundishayo,

18kwa maana inapendeza unapoyahifadhi moyoni mwako

na kuwa nayo yote tayari mdomoni mwako.

19Ili tumaini lako liwe katika Bwana ,

hata wewe, ninakufundisha leo.

20Je, sijakuandikia misemo thelathini,

misemo ya mashauri na maarifa,

21kukufundisha maneno ya kweli na ya kuaminika,

ili uweze kutoa majibu sahihi

kwake yeye aliyekutuma?

22Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini,

wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,

23kwa sababu Bwana atawatetea

naye atawateka hao waliowateka.

24Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka,

usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,

25la sivyo utajifunza njia zake

na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.

26Usiwe mwenye kupeana mikono katika rehani,

au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni;

27ukikosa njia ya kulipa,

kitanda chako kitachukuliwa

ukiwa umekilalia.

28Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani

lililowekwa na baba zako.

29Je, unamwona mtu stadi katika kazi yake?

Atahudumu mbele ya wafalme;

hatahudumu mbele ya watu duni.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.