Mithali 25

Mithali 25

Mithali zaidi za Sulemani

1Hizi ni mithali zaidi za Sulemani, zilizonakiliwa na watumishi wa Hezekia mfalme wa Yuda:

2Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo,

bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.

3Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini,

ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.

4Ondoa takataka kwenye madini ya fedha,

na ndani yake kutatokea chombo

cha mfua fedha.

5Ondoa waovu mbele ya mfalme,

nacho kiti chake cha ufalme

kitaimarishwa kupitia kwa haki.

6Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme,

wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu;

7ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,”

kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu.

Kile ulichokiona kwa macho yako

8usiharakishe kukipeleka mahakamani,

maana utafanya nini mwishoni

kama jirani yako atakuaibisha?

9Ukifanya shauri na jirani yako,

usisaliti siri ya mtu mwingine,

10ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha,

na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.

11Neno lisemwalo kwa wakati ufaao

ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu

yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.

12Kama vile kipuli cha dhahabu

au pambo la dhahabu safi,

ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima

kwa sikio lisikilizalo.

13Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno

ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao,

huburudisha roho za bwana zake.

14Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua

ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.

15Kwa uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa,

nao ulimi laini unaweza kuvunja mfupa.

16Ukipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha,

ukila zaidi, utatapika.

17Nenda nyumbani mwa jirani yako mara chache;

ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.

18Kama vile rungu au upanga au mshale mkali

ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.

19Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa,

ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.

20Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi,

au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi,

ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.

21Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale;

kama ana kiu, mpe maji anywe.

22Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto

yanayowaka kichwani pake,

naye Bwana atakupa thawabu.

23Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua,

ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.

24Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,

kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.

25Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka

ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.

26Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au

kisima kilichotiwa taka

ndivyo alivyo mtu mwenye haki

akishiriki na waovu.

27Si vyema kula asali nyingi sana,

wala si heshima

kujitafutia heshima yako mwenyewe.

28Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka

ndivyo alivyo mtu

ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.