The chat will start when you send the first message.
1Hekima amejenga nyumba yake;
amechonga nguzo zake saba.
2Ameandaa nyama na kuchanganya divai yake;
pia ameandaa meza yake.
3Amewatuma wajakazi wake, naye huita
kutoka mahali pa juu sana pa mji.
4Anawaambia wale wasio na akili,
“Wote ambao ni wajinga na waje hapa!
5Njooni, mle chakula changu
na mnywe divai niliyoichanganya.
6Acheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi;
tembeeni katika njia ya ufahamu.
7“Yeyote anayemkosoa mwenye dhihaka
hukaribisha matusi;
yeyote anayekemea mtu mwovu
hupatwa na matusi.
8Usimkemee mwenye dhihaka, la sivyo atakuchukia;
mkemee mwenye hekima naye atakupenda.
9Mfundishe mtu mwenye hekima
naye atakuwa na hekima zaidi;
mfundishe mtu mwadilifu
naye atazidi kufundishika.
10“Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,
na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.
11Kwa maana kwa msaada wangu
siku zako zitakuwa nyingi,
na miaka itaongezwa katika maisha yako.
12Kama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo;
kama wewe ni mtu wa mzaha,
wewe mwenyewe ndiwe utateseka.”
13Mwanamke aitwaye Mpumbavu ana kelele;
hana adabu na hana maarifa.
14Huketi kwenye mlango wa nyumba yake,
kwenye kiti katika mahali pa juu sana pa mji,
15akiita wale wanaopita karibu,
wanaoenda moja kwa moja kwenye njia yao.
16Anawaambia wale wasio na akili,
“Wote ambao ni wajinga na waje hapa ndani!
17Maji yaliyoibiwa ni matamu;
chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!”
18Lakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo,
kwamba wageni wake huyo mwanamke
wako katika vilindi vya Kuzimu.