The chat will start when you send the first message.
1Ee Bwana , sikia na unijibu,
kwa maana mimi ni maskini na mhitaji.
2Linda maisha yangu, kwa maana nimejiweka kwako,
wewe ni Mungu wangu,
mwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
3Ee Bwana, nihurumie mimi,
kwa maana ninakuita mchana kutwa.
4Mpe mtumishi wako furaha,
kwa kuwa kwako wewe, Ee Bwana,
ninainua nafsi yangu.
5Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe,
umejaa upendo kwa wote wakuitao.
6Ee Bwana , sikia maombi yangu,
sikiliza kilio changu unihurumie.
7Katika siku ya shida yangu nitakuita,
kwa maana wewe utanijibu.
8Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe,
hakuna matendo ya kulinganishwa na yako.
9Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya
yatakuja na kuabudu mbele zako;
wataliletea utukufu jina lako.
10Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu;
wewe peke yako ndiwe Mungu.
11Ee Bwana , nifundishe njia yako,
nami nitaenda katika kweli yako;
nipe moyo usiositasita,
ili niweze kulicha jina lako.
12Ee Bwana Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wote;
nitaliadhimisha jina lako milele.
13Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu;
umeniokoa kutoka vilindi vya kaburi.
14Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia;
kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu:
watu wasiokuheshimu wewe.
15Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema,
si mwepesi wa hasira,
bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.
16Nigeukie na unihurumie;
mpe mtumishi wako nguvu zako,
mwokoe mwana wa mjakazi wako.
17Nipe ishara ya wema wako,
ili adui zangu waione nao waaibishwe,
kwa kuwa wewe, Ee Bwana ,
umenisaidia na kunifariji.