The chat will start when you send the first message.
1Mpenzi wako ameenda wapi,
ewe mzuri kupita wanawake wote?
Mpenzi wako amegeukia njia ipi,
tupate kumtafuta pamoja nawe?
2Mpenzi wangu ameenda bustanini mwake,
kwenye vitalu vya vikolezo,
kujilisha bustanini
na kukusanya yungiyungi.
3Mimi ni wake mpenzi wangu,
na mpenzi wangu ni wangu;
yeye hujilisha kati ya yungiyungi.
4Wewe ni mzuri, mpendwa wangu, kama Tirsa,
unapendeza kama Yerusalemu,
umetukuka kama jeshi lenye bendera.
5Uyageuze macho yako mbali nami;
yananigharikisha.
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi
wanaoteremka kutoka Gileadi.
6Meno yako ni kama kundi la kondoo
wanaotoka kuogeshwa.
Kila mmoja ana pacha lake,
hakuna hata mmoja aliye peke yake.
7Mashavu yako nyuma ya shela yako
ni kama vipande viwili vya komamanga.
8Panaweza kuwa na malkia sitini,
masuria themanini,
na mabikira wasiohesabika;
9lakini hua wangu, mkamilifu wangu,
ni wa namna ya pekee,
binti pekee kwa mama yake,
kipenzi cha yeye aliyemzaa.
Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa;
malkia na masuria walimsifu.
10Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko,
mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua,
ametukuka kama nyota zinazofuatana?
11Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi
ili kutazama machipuko ya bondeni,
kuona kama mizabibu imechipua
au kama mikomamanga imechanua maua.
12Kabla sijangʼamua,
shauku yangu iliniweka
katikati ya magari ya vita ya wakuu wangu.
13Rudi, rudi, ee Mshulami;
rudi, rudi ili tupate kukutazama!
Kwa nini kumtazama Mshulami,
kama kutazama ngoma ya Mahanaimu?