2 Mambo ya Nyakati 28

2 Mambo ya Nyakati 28

Utawala wa Ahazi

1Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; wala hakufanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, kama Daudi babaye;[#2 Fal 16:2]

2bali akaziendea njia za wafalme wa Israeli, alitengeneza sanamu za mabaali za kusubu.[#Kut 34:17; Law 19:4; Amu 2:11]

3Tena akafukiza uvumba katika bonde la mwana wa Hinomu, akawateketeza wanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli.[#2 Fal 23:10; Yer 7:31; Law 18:21; 2 Fal 16:3; 2 Nya 33:6; Eze 16:20; Mik 6:7]

4Akatoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na vilimani, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.

Shamu na Israeli waishinda Yuda

5Kwa hiyo BWANA, Mungu wake, akamtia mkononi mwa mfalme wa Shamu; wakampiga, wakawachukuwa watu wake wengi sana mateka, wakawaleta Dameski. Tena akatiwa mkononi mwa mfalme wa Israeli, aliyempiga mapigo makuu.[#Isa 7:1; 2 Fal 16:5]

6Peka mwana wa Remalia akawaua katika Yuda siku moja watu elfu mia moja na ishirini, mashujaa wote; kwa sababu walikuwa wamemwacha BWANA, Mungu wa baba zao.[#2 Fal 15:27; Isa 9:21; Yos 23:16; Yer 2:19]

7Naye Zikri, mtu hodari wa Efraimu, akawaua Maaseya mwana wa mfalme, na Azrikamu mkuu wa nyumba, na Elkana, aliyekuwa wa pili wake mfalme.

Obedi aingilia kati

8Waisraeli wakachukua mateka ndugu zao wafungwa elfu mia mbili wakiwemo wanawake, watoto wa kiume na kike, pia wakachukua kwao nyara nyingi, wakazileta nyara Samaria.[#2 Nya 11:4]

9Lakini kulikuwako huko nabii wa BWANA, jina lake aliitwa Odedi; akatoka kuwalaki jeshi waliokuja Samaria, akawaambia, Angalieni, kwa kuwa BWANA, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, yeye amewatia mikononi mwenu, nanyi mmewaua kwa ghadhabu iliyofikia mbinguni.[#Amu 3:8; Zab 69:26; Isa 10:5; 47:6; Eze 25:12,15; 26:2; Oba 1:10; Zek 1:15; Mwa 4:10; 11:4; Ezr 9:6; Ufu 18:5]

10Na sasa mnanuia kuwatawala wana wa Yuda na Yerusalemu na kuwafanya wawe watumwa na wajakazi wenu; lakini ninyi nanyi je! Hamna hatia zenu wenyewe juu ya BWANA, Mungu wenu?[#Law 25:39; Yer 25:29; 1 Pet 4:17]

11Haya, nisikieni mimi basi, mwarudishe wafungwa, mliowachukua mateka wa ndugu zenu; kwa maana ghadhabu ya BWANA iliyo kali iko juu yenu.[#Yak 2:13]

12Ndipo wakaondoka juu ya hao waliotoka vitani baadhi ya wakuu wa wana wa Efraimu, Azaria, mwana wa Yohanani, na Berekia mwana wa Meshilemothi, na Yehizkia mwana wa Shalumu, na Amasa mwana wa Hadlai,

13wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za BWANA, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli.[#Hes 32:14; Yos 22:17]

14Basi watu wenye silaha wakawaachilia wafungwa na nyara mbele ya wakuu na kusanyiko lote.

15Wakaondoka wale watu waliotajwa majina yao, wakawatwaa wafungwa, wakawavika kwa zile nyara wale wote waliokuwa uchi, wakawapa mavazi na viatu, wakawalisha, wakawanywesha, wakawatia mafuta, wakawapandisha waliokuwa dhaifu miongoni mwao juu ya punda wakawaleta Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wakarudi Samaria.[#2 Fal 6:22; Mt 25:21,22; Lk 6:27; Rum 12:20; Kum 34:3; Amu 1:16]

Ashuru Yakataa Kuisaidia Yuda

16Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie.[#2 Fal 16:7; Isa 7:1-9; #28:16 Kiebrania ‘Wafalme wa Ashuru’.]

17Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa.[#Law 26:18]

18Wafilisti pia walikuwa wameishambulia na kuitwaa miji ya Shemeshi, Ayaloni, Gederothi, soko, pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake na Gimzo pia na vijiji vyake, miji yake; wakakaa humo.[#Yos 15:22; Eze 16:27,57]

19Kwa maana BWANA aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi BWANA mno.[#2 Nya 21:2; Kut 32:25; Ufu 3:17; 16:15]

20Na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru akamjia, akamfadhaisha, asimtie nguvu kwa lolote.[#2 Fal 15:29; 16:7-9; Isa 7:20]

21Kwa maana Ahazi alitwaa sehemu katika nyumba ya BWANA, na katika nyumba ya mfalme, na ya wakuu, akampa mfalme wa Ashuru; asisaidiwe na jambo hilo.

Ukaidi na kifo cha Ahazi

22Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi BWANA, huyo mfalme Ahazi.[#2 Nya 33:12; Zab 50:15; Isa 1:5; Yer 5:3; Hos 5:15; Ufu 16:11]

23Maana aliitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote.[#2 Nya 25:14; Yer 44:17,18]

24Tena Ahazi akakusanya vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, akavikata vipande vipande vyombo vya nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya nyumba ya BWANA; akajijengea madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu.[#2 Nya 29:3,7]

25Na katika kila mji wa Yuda akafanya mahali pa juu pa kuifukizia miungu mingine uvumba, akamkasirisha BWANA, Mungu wa babaze.

26Basi mambo yake yote yaliyosalia, na njia zake zote, za kwanza hadi za mwisho, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda na Israeli.[#2 Fal 16:19,20; 2 Nya 20:34; 27:7-9]

27Ahazi akalala na babaze, wakamzika mjini, yaani, Yerusalemu; maana hawakumleta makaburini mwa wafalme wa Israeli; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania