The chat will start when you send the first message.
1Elisha akasema, Lisikieni neno la BWANA; BWANA asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.[#Kut 8:23; Yos 3:5; Zab 46:1]
2Basi yule afisa, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama BWANA angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.[#2 Fal 5:18; Mwa 7:11; 8:2; Mal 3:10; Kum 3:27; Ebr 3:17]
3Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe?[#Law 13:46; Hes 5:2; Kum 24:8,9; 2 Fal 5:27; Lk 17:12]
4Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu.[#Est 4:16; Lk 15:17-19]
5Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kambi ya Washami, kumbe! Hapakuwa na mtu.
6Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi.[#Law 26:36; 2 Sam 5:24; 2 Fal 3:23; 19:7; Ayu 15:21; Eze 10:5; Ufu 6:15,16; 1 Fal 10:29]
7Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kambi yao vile vile kama ilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao.[#Ayu 18:11; Zab 48:4-6; 53:5; Mit 28:1; Yer 48:8,9]
8Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha.
9Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme.[#Flp 2:14; 2 Pet 1:19; Est 9:17; Isa 41:27; Nah 1:15; Hes 32:23]
10Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu yeyote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha.
11Na mabawabu wakaita, wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.
12Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha shambani, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini.
13Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kumradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone.
14Basi wakatwaa magari mawili na farasi wake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Nendeni, mkaangalie.
15Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme.
16Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la BWANA.[#Hes 23:19; Zab 89:2; 119:89; Isa 40:8; 44:26; Mt 24:35; Mk 13:31; 1 Kor 1:9; 1 The 5:24; 1 Pet 1:25]
17Naye mfalme akamweka yule ofisa mlinzi, ambaye alitegemea mkono wake, awasimamie watu langoni; na watu wakamkanyaga langoni, akafa; kama alivyosema yule mtu wa Mungu, aliyenena hapo mfalme alipomshukia.[#Kum 32:35-40; 2 Fal 6:32; 2 Nya 36:16; Ayu 21:28-30; Zab 31:17,18; Mit 13:13; Isa 5:24; Lk 10:16; 1 The 4:8; Ebr 10:30,31; Yud 1:14,15]
18Ikatukia kama vile yule mtu wa Mungu alivyomwambia mfalme, Vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, na kipimo cha unga mzuri kwa shekeli, ndivyo vitakavyokuwa kesho, panapo saa hii, katika lango la Samaria;[#2 Fal 7:1]
19na yule kiongozi akamjibu mtu wa Mungu, akasema, Sasa tazama, kama BWANA angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akasema, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.
20Ikampata vivyo hivyo, kwa kuwa watu walimkanyaga langoni, akafa.[#Hes 20:12; Ayu 20:23; Yer 17:6; Ebr 3:18]