The chat will start when you send the first message.
1Makuhani Walawi, kabila yote ya Lawi, wasiwe na fungu wala urithi pamoja na Israeli; watakula sadaka za BWANA zifanywazo kwa moto, na urithi wake.[#Hes 18:8,9; 1 Kor 9:13]
2Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; BWANA ndiye urithi wao, kama alivyowaambia.[#Hes 18:20]
3Na hii itakuwa haki ya makuhani kwa watu hao wasongezao sadaka, ikiwa ni ng'ombe au kondoo wampe kuhani mkono, na mashavu mawili, na tumbo.[#Law 7:30]
4Malimbuko ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na manyoya ya kwanza ya kondoo wako, umpe.[#Kut 22:29; Hes 18:12]
5Kwani BWANA, Mungu wako, amemchagua katika kabila zako zote, asimame atumike kwa jina la BWANA, yeye na wanawe milele.[#Kum 10:8]
6Na akija Mlawi atokaye katika malango yako mojawapo, katika Israeli yote alipokuwa akikaa, akaja kwa mapenzi yote ya nafsi yake mahali atakapochagua BWANA;[#Hes 35:2,3]
7na atumike kwa jina la BWANA, Mungu wake, kama wafanyavyo ndugu zake wote, Walawi wasimamao huko mbele za BWANA.
8Wawe na fungu sawasawa la kula, pamoja na haya yaliyomfikia kwa kuuzwa urithi wa baba zake.[#2 Nya 31:4; Neh 12:44]
9Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale.[#Law 18:26; Kum 12:29]
10Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,[#Law 19:26; Kut 22:18]
11wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.[#Law 19:31]
12Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.[#Law 18:24]
13Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako.[#Mt 5:48; Mwa 17:1]
14Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, BWANA, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.[#2 Fal 21:6]
15BWANA, Mungu wako, atakupa nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye.[#Mdo 3:22; 7:37; Hes 24:17; Isa 11:1; 61:1; Mt 11:3; 21:11; Lk 2:25-34; 4:16-22; Lk 7:16; 24:19; Yn 4:19-26; 6:14; 7:40]
16Kama vile ulivyotaka kwa BWANA, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya BWANA, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa.
17BWANA akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema.
18Mimi nitawainulia nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.[#Yn 1:45; Isa 51:16; Yn 17:8; 4:25; 8:28; 12:49,50]
19Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.[#Mdo 3:23]
20Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.[#Kum 13:5; Yer 14:14; Zek 13:3; Yer 2:8]
21Nawe ukisema moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena BWANA?
22Atakaponena nabii kwa jina la BWANA, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena BWANA; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope.[#Yer 28:9]