Kutoka 18

Kutoka 18

Yethro Amshauri Musa

1Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli watoke Misri.

2Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha,[#Kut 2:21-22]

3pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi za kigeni;[#Mdo 7:29; #18:3 Katika Kiebrania ni mgeni au mkimbizi.]

4na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao.[#18:4 Katika Kiebrania ‘Eli’ ina maana ya ‘Mungu wangu’ na ‘Ezeri’ lina maana ya ‘msaada’.]

5Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepiga kambi, kwenye mlima wa Mungu;

6naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye.

7Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akamwinamia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.

8Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa.

9Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyowaokoa mikononi mwa Wamisri.

10Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri.

11Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa ujeuri.[#2 Nya 2:5; Zab 95:3; 97:9; Isa 37:16-20; Dan 2:47; Ayu 40:11; Lk 1:51]

12Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.[#Kum 12:7; 1 Kor 10:18,21,31]

13Asubuhi yake Musa akaketi ili awaapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni.

14Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni?

15Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu;

16wakiwa na neno, hunijia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajulisha amri za Mungu, na sheria zake.[#2 Sam 15:3; Ayu 31:13; Hes 36:6]

17Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.

18Kwa kweli utajidhoofisha mwenyewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako.[#Hes 11:14; Kum 1:9,12]

19Sikiliza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; wewe uwe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao;[#Kum 5:5; Hes 27:5]

20nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya.[#Kum 4:1,5; Zab 143:8; Kum 1:18]

21Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mamia, na wakuu wa hamsini hamsini, na wakuu wa kumi kumi;[#Kum 16:18; Mdo 6:3; Mwa 42:18; 2 Sam 23:3; Eze 18:8]

22nao wawaamue watu hawa siku zote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe.[#Law 24:11; Hes 15:33; Kum 17:8]

23Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani.

24Basi Musa akalisikiliza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia.

25Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mamia, na wakuu wa hamsini hamsini, na wakuu wa kumi kumi.[#Kum 1:15; Mdo 6:5]

26Nao wakawaamua watu siku zote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe.[#Ayu 29:16]

27Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.[#Hes 10:29]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania