Wagalatia 2

Wagalatia 2

Paulo na mitume mengine

1Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami.[#Mdo 11:30; 15:2]

2Nami nilikwenda kwa kuwa nilifunuliwa, nikawaeleza Injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao viongozi waliosifika, isiwe labda napiga mbio bure, au nilipiga mbio bure.[#Gal 6:9]

3Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Mgiriki, hakulazimishwa kutahiriwa.[#Mdo 16:3]

4Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani;[#Mdo 15:1,24]

5ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi.[#Gal 3:1]

6Lakini wale viongozi waliosifika kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyovyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao waliosifika hawakuniongezea kitu;[#Kum 10:17]

7bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa Injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro alivyokabidhiwa ya waliotahiriwa;[#Mdo 9:15; 15:12; 22:21]

8(maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa);

9tena Yakobo, Kefa, na Yohana, waliosifika kuwa ni nguzo, walipoitambua ile neema niliyopewa, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kulia wa kuonesha ushirikiano; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;[#Yn 1:42]

10ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nilikuwa na bidii kulifanya.[#Mdo 11:30; 12:25]

Paulo amkemea Petro huko Antiokia

11Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nilishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu.

12Kwa maana kabla hawajaja watu kadhaa waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini hao walipokuja, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa.[#Mdo 11:3]

13Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao.

14Lakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nilimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi?

Wayahudi na Mataifa huokolewa kwa imani

15Sisi tulio Wayahudi kwa asili, wala si wa Mataifa wenye dhambi,

16Lakini tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.[#Zab 143:2; Rum 3:20,22,28; 4:5; 11:6; Mdo 15:10,11; Efe 2:8]

17Lakini ikiwa sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha!

18Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonesha ya kuwa mimi mwenyewe ni mkosaji.

19Maana mimi kwa njia ya sheria niliifia sheria ili nimwishie Mungu.[#Rum 7:6]

20Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.[#Yn 13:1; 17:23; 1 Yoh 3:16; Gal 1:4]

21Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania