Mwanzo 21

Mwanzo 21

Kuzaliwa kwa Isaka

1BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema.[#1 Sam 2:21; Mwa 17:19; 18:10; Gal 4:23]

2Sara akapata mimba akamzalia Abrahamu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu.[#Ebr 11:11; Mdo 7:8]

3Abrahamu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia.[#Mwa 17:19]

4Abrahamu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru.[#Mwa 17:12; Mdo 7:8]

5Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka mia moja, alipozaliwa mwana wake Isaka.

6Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami.[#Zab 126:2; Isa 54:1; Lk 1:14,58]

7Akasema, Ni nani angemwambia Abrahamu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake.[#Mwa 18:11]

Hajiri na Ishmaeli wafukuzwa

8Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Abrahamu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya.

9Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Abrahamu, anafanya dhihaka.[#Mwa 16:1,4,15; Gal 4:29]

10Kwa hiyo akamwambia Abrahamu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.[#Gal 4:29-30; Mwa 25:6; 36:6,7]

11Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Abrahamu, kwa ajili ya mwanawe.[#Mwa 17:18]

12Mungu akamwambia Abrahamu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.[#Rum 9:7; Ebr 11:18]

13Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.[#Mwa 16:10; 17:20; 25:12]

14Abrahamu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akamtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.[#Yn 8:35]

15Yale maji yalipoisha katika kiriba, Hajiri akamlaza kijana kichakani.[#Hes 20:5; Zab 63:1]

16Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.[#Mwa 44:34]

17Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.[#Kut 3:7; 2 Fal 13:4,23]

18Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.[#Mwa 21:13; 25:12; Amu 8:24]

19Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.[#Hes 22:31; 2 Fal 6:17; Lk 24:16]

20Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.[#Mwa 16:12; 39:2,3]

21Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.[#Mwa 24:4; 20:2; 26:28; Isa 8:10]

Abrahamu na Abimeleki wawekeana agano

22Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Abrahamu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda.[#Mwa 26:26]

23Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake.[#Yos 2:12; 1 Sam 24:21]

24Abrahamu akasema, Nitaapa.

25Kisha Abrahamu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki wamemnyang'anya.[#Mwa 26:15-22]

26Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu.

27Abrahamu akatwaa kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano.[#Mwa 26:28-31]

28Abrahamu akawaweka wana-kondoo majike saba peke yao.

29Abimeleki akamwuliza Abrahamu, Hawa wana-kondoo saba majike, uliowaweka, maana yake ni nini?[#Mwa 33:8]

30Akasema, Hawa wana-kondoo saba majike utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki.[#Mwa 31:48]

31Kwa hiyo akapaita mahali pale Beer-sheba, kwa sababu waliapa huko wote wawili.[#Mwa 26:33]

32Basi wakafanya mapatano huko Beer-sheba. Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakaondoka wakarudi hata nchi ya Wafilisti.[#Yos 13:2]

33Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaliitia huko jina la BWANA Mungu wa milele.[#Kum 33:27; Zab 9:7; Isa 9:6; Rum 16:26; Ebr 13:8; 1 Tim 1:17; Ufu 10:6]

34Abrahamu akaishi kama mgeni kwa Wafilisti siku nyingi.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania