Mwanzo 41

Mwanzo 41

Yusufu afasiri ndoto ya Farao

1Ikawa, baada ya miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto.

2Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini.

3Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto.

4Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka.

5Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.

6Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

7Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu.

8Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.[#Dan 1:20; 2:2; 4:5; Kut 7:11; Isa 29:14; Mt 2:1]

9Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo.

10Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari walinzi, mimi na mkuu wa waokaji.[#Mwa 39:20; 40:2,3]

11Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota.[#Mwa 40:5]

12Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake.[#2 Fal 5:4; Mwa 37:36; 40:12]

13Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nilirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa.[#Mwa 40:22]

14Ndipo Farao akatuma watu kumwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao.[#Zab 105:20; 113:7,8; Dan 2:25; 1 Sam 2:8]

15Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.[#Zab 25:14; Dan 5:16]

16Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani.[#Zab 25:14; Mit 3:32; Dan 2:30; 4:2; Amo 3:7; Yn 15:15; Mdo 3:12; 2 Kor 3:5; Kum 29:29]

17Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa mto;

18na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha nyasini.

19Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu.

20Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono.

21Na walipowala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka.

22Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa.

23Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

24Na hayo masuke dhaifu yakayala yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionesha maana yake.[#Zab 60:11; 118:8; Isa 8:19; Dan 4:7]

25Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibuni.[#Dan 2:28,29,45; Ufu 4:1]

26Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja.

27Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa.[#2 Fal 8:1]

28Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibuni.

29Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.

30Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi.[#Mwa 47:13; Zab 105:16; 1 Fal 17:1]

31Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa kali sana.

32Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.

33Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri.

34Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba.

35Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji.

36Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.

37Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumishi wake wote.

38Farao akawaambia watumishi wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye Roho ya Mungu ndani yake?[#Hes 27:18; Mit 2:6; Ayu 32:8; Dan 4:8; 5:11]

39Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.

40Basi wewe utakuwa msimamizi wa nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.[#Mdo 7:10]

41Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.[#Zab 105:22; Mit 14:35; Mhu 4:13,14; Dan 6:3; Mdo 7:10]

42Farao akavua pete yake ya mhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.[#Dan 5:29; Est 3:10; 8:2]

43Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri.

44Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.

45Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe. Na Yusufu akaenda huku na huko katika nchi yote ya Misri.

46Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akasafiri katika nchi yote ya Misri.[#1 Sam 16:21; 1 Fal 12:6,8; Dan 1:19]

47Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ilitoa mazao mengi kabla ya kuja kwa miaka ya njaa.

48Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake.

49Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu.[#Mwa 22:17; Amu 7:12; 1 Sam 13:5; Zab 78:27]

50Kabla ya kuja miaka ya njaa, Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili.[#Mwa 46:20; 48:5]

51Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu.

52Na wa pili akamwita jina lake Efraimu, maana alisema, Mungu amenipa uzazi katika nchi ya mateso yangu.

53Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri,

54ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula.[#Mdo 7:11; Zab 105:16]

55Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Nendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni.[#Yn 2:5]

56Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri.[#Mwa 42:6; 47:14,24; Mit 11:26]

57Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.[#Kum 9:28; Mwa 12:10; 26:1; 43:1; 2 Fal 8:1]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania