Isaya 9

Isaya 9

Utawala wa haki wa mfalme Ajaye

1Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo awali aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa.[#Mt 4:15; 2 Fal 15:29; 2 Nya 16:4; Law 26:24; 1 Nya 5:26]

2Watu wale waliokwenda katika giza[#Isa 50:10; Yn 8:12; Efe 5:8; Mt 4:16; Lk 1:79]

Wameona nuru kuu;

Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti,

Nuru imewaangaza.

3Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao;

Wanafurahi mbele zako,

Kama furaha ya wakati wa mavuno,

Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara.

4Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani.[#Amu 7:22; Zab 83:9; Isa 10:26]

5Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyovingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni.

6Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,[#Lk 2:11; Yn 3:16; Mt 28:18; 1 Kor 15:25; Amu 13:18; Zab 45:3,6; Yer 23:6; Yn 1:1; Tit 2:13; Efe 2:14; Kol 1:20; Ebr 13:20]

Tumepewa mtoto wa kiume;

Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake;

Naye ataitwa jina lake,

Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,

Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.

7Mamlaka ya enzi yake yatakuzwa daima,[#Dan 2:44; Lk 1:32-33]

Na kutakuwa na amani isiyo na mwisho,

Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake;

Kuuthibitisha na kuutegemeza

Kwa hukumu na kwa haki,

Tangu sasa na hata milele.

Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.

Hukumu kwa ujeuri na udhalimu

8Bwana alimpelekea Yakobo neno, nalo likamfikia Israeli.

9Nao watu wote watajua, yaani, Efraimu na yeye akaaye Samaria, wasemao kwa kiburi na kwa kujisifu nafsi zao,

10Matofali yameanguka, lakini sisi tutajenga kwa mawe yaliyochongwa; mikuyu imekatwa lakini sisi tutaweka mierezi badala yake.

11Kwa sababu hiyo BWANA atawainua adui wa Resini juu yake, naye atawachochea adui zake;

12Waashuri upande wa mbele, na Wafilisti upande wa nyuma, nao watamla Israeli kwa kinywa kilicho wazi. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.

13Lakini watu hao hawakumwelekea yeye aliyewapiga, wala kumtafuta BWANA wa majeshi.[#Yer 5:3]

14Kwa sababu hiyo BWANA atakata katika Israeli kichwa na mkia, kuti na nyasi, katika siku moja.

15Mzee mwenye kuheshimiwa ndiye kichwa, na nabii afundishaye uongo ndiye mkia.

16Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia.

17Kwa sababu hiyo Bwana hatawafurahia vijana wao, wala hatawahurumia yatima wao wala wajane wao; maana kila mtu ni mnajisi, dhalimu, na kila ulimi hunena upumbavu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.

18Kwa maana uovu huteketeza kama moto; huila mibigili na miiba, naam, huwaka katika vichaka vya mwitu, nao hupaa juu katika mawingu mazito ya moshi.

19Kwa sababu ya hasira ya BWANA wa majeshi nchi hii inateketea kabisa; watu hawa nao ni kama kuni zitiwazo motoni; hapana mtu amhurumiaye ndugu yake.

20Hupokonya upande wa mkono wa kulia, nao huona njaa! Hula upande wa mkono wa kushoto, wala hawashibi! Watakula kila mtu nyama ya mkono wake mwenyewe.[#Law 26:26]

21Manase anamla Efraimu, naye Efraimu anamla Manase; nao wawili pamoja watakuwa juu ya Yuda. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania