Yoshua Mwana wa Sira 12

Yoshua Mwana wa Sira 12

Fadhili

1Utoapo fadhili, uwe na hakika ya mtu umfadhiliye; na fadhili zako zitakuta shukrani.[#Mt 7:6]

2Umfadhili mwenye akili, nawe utaona thawabu; kama si kwake yeye, utaipata kwake Aliye Juu.

3Hakuna mema yatakayomjia yule anayeendelea katika maovu, wala mtu yule asiyetoa sadaka.

4Basi mpe mwenye adili, usimsaidie mwenye dhambi;

5mfadhili mnyonge, usimpe asiye haki chochote; hata chakula umnyime usimpe, asije akakuangamiza hivyo; kwa kuwa utapokea mabaya maradufu badala ya mema yote uliyomtendea.

6Naam, Aliye Juu huchukizwa na wenye dhambi, naye atajilipiza kisasi juu yao wasio haki.

7Basi, mpe mtu mwema, usimsaidie mwenye dhambi.

Marafiki wa Kweli na wa Uongo

8Rafiki wa mtu hajaribiwi wakati wa heri, wala adui yake hafichiki wakati wa shari.

9Mtu akiona heri hata adui zake watakuwa ni rafiki; akipatwa na shari hata rafiki yake aweza kufarakana naye.

10Usimtegemee adui yako, maana kama kutu ya shaba ndivyo ulivyo ubaya wake;

11ingawa amejidhili na kuigandama nchi, uangalie na kujihadhari naye; (utakuwa kwake mfano wa mtu anayeupangusa upatu, na kujua ya kwamba kutu ikalipo).

12Huyo usimweke karibu nawe, asije akakuondoa akasimama mahali pako; usimketishe mkono wa kuume asije akatafuta kukichukua kiti chako. Hatimaye utayakiri maneno yangu, na kuchomwa kwa mithali zangu.

13Ni nani atakayemhurumia mganga aliyeumwa na nyoka wake? Au mtu yeyote ambaye huwakaribia wanyama wakali?

14Vivyo hivyo ni nani atakayemhurumia mtu amwendeaye mkosaji, na kushirikiana naye katika dhambi zake?

15Muda kitambo atakaa nawe lakini mara ukipungua nguvu yeye hatadumu;

16mradi adui atabembeleza kwa midomo yake, bali moyoni mwake anafanya shauri jinsi ya kukuangusha shimoni; aidha, adui atatoka machozi machoni pake, bali akiona nafasi haitamtosha damu yako.

17Ukipatwa na shari, utamwona papo hapo amekutangulia; na kana kwamba anataka kukusaidia atakupiga akumalize.

18Naye atatikisa kichwa, na kupiga makofi, na kunong'ona tele, na kubadili uso wake.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania