Yoshua Mwana wa Sira 3

Yoshua Mwana wa Sira 3

Wajibu kwa Wazazi

1Wanangu, mnisikilize mimi, baba yenu, na kutenda kama haya, ili mfanikiwe.

2Madhali BWANA amempa baba utukufu kuhusu wana, na kuithibitisha haki ya mama kuhusiana na watoto.

3Amheshimuye baba yake atafanya upatanisho wa dhambi,

4naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo azizi.

5Amheshimuye babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa.

6Amtukuzaye baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza BWANA, atamstarehesha mamaye,

7na kuwatumikia wazazi wake kama mabwana.

8Katika neno na katika tendo umheshimu baba yako, ili baraka zote zikujie kutoka kwake.[#Kut 20:12]

9Mradi baraka ya baba itaziimarisha nyumba zao watoto, bali laana ya mama huing'oa misingi.

10Usijisifu hata kumwaibisha baba yako, maana aibu ya baba yako siyo utukufu wako.

11Utukufu wa mtu ndio utokao katika heshima ya baba yake, na mama aliyefedheheka ni lawama ya watoto wake.

12Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake.

13Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana;

14kwa maana sadaka apewayo baba haitasahauliwa, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukuthibitisha;

15siku ya msiba wako itakumbukwa juu yako; kama jua kali juu ya sakitu, ndivyo dhambi zako zitakavyoyeyuka.

16Mwenye kumdharau baba yake ni mfidhuli, naye mwenye kumlaani mama yake amekwisha kulaaniwa na BWANA.

Unyenyekevu

17Mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa kuliko mweye ukarimu.

18Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekeza,[#Flp 2:3]

19nawe utapata kibali machoni pa BWANA;

20kwa maana rehema zake BWANA ni kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu.

21Usiyatafute mambo ya ajabu ya kukushinda, wala kuyachunguza yaliyositirika kwako.

22Yale uliyoagizwa uyatafakari, huna haja ya mambo yaliyofichwa.[#Kum 29:29]

23Usijishughulishe na mambo yasiyodirikika, maana umekwisha kuoneshwa mengi zaidi kuliko watu wawezavyo kufahamu.

24Lakini majivuno ya wanadamu ni mengi,

na mawazo ya upuzi yawaongoza watu kunako ukosefu.

25Bila mboni ya jicho hakuna nuru,

Wala hakuna hekima bila ufahamu.

Kiburi

26Moyo mgumu utapata kisirani halafu,

Bali apendaye mema atakwenda nayo.

27Moyo mgumu utazidishiwa mashaka,

Na mkosaji hujirundikia dhambi juu ya dhambi.

28Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona,

Mche wa uovu umepandwa ndani yake.

29Moyo wa busara utatambua mithali,

Na sikio sikivu ni tamaa ya mtaalamu.

Sadaka kwa Maskini

30Maji huuzimisha moto uwakao,

Na sadaka huwa upatanisho wa dhambi.

31Alipaye hisani itamkuta njiani,

Na wakati wa kuanguka atapata nguzo.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania