Yoshua Mwana wa Sira 35

Yoshua Mwana wa Sira 35

Sheria na Dhabihu

1Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuziangalia amri ndiye aitoaye kafara ya amani;

2amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora; naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabihu ya kushukuru.

3Kuuacha uovu kwampendeza BWANA, na kujitenga na udhalimu ni kipatanisho.

4Lakini ujihadhari usitokee mbele za BWANA mikono mitupu; maana sharti hayo yote yatendeke kwa ajili ya amri.

5Toleo lake mwenye haki lina kibali madhabahuni, na harufu yake tamu, yafika mbele zake Aliye Juu.

6Dhabihu ya mwenye haki yakubalika, wala kumbukumbu lake halisahauliki.

7Umheshimu BWANA kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili.

8Kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko.

9Mpe Mungu kama alivyokupa wewe; na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu.[#2 Kor 9:7]

10Amhurumiaye maskini humkopesha BWANA, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni Yeye; kwa kuwa BWANA hulipa, naye atakulipa wewe mara saba.

Haki ya Mungu

11Usidhanie kuwa unaweza kutoa rushwa, kwa maana Yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri,

12kwa kuwa BWANA ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu.

13Hatamkubali yeyote juu ya maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa.

Haki ya Mungu

14Hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake.

15Je! Machozi ya mjane hayachuruziki mashavuni mwake? Naye aziugulia taabu zake zilizoyatokeza.

16Malalamiko yake aliyeonewa yatapata kukubaliwa, na dua yake itafika hima mbinguni.

17Sala yake mnyenyekevu hupenya mawingu; wala haitatulia hata itakapowasili;

18wala haitaondoka hata Aliye Juu atakapoiangalia, akaamua kwa adili, akatekeleza hukumu.

19Wala BWANA hatalegea, wala hatakuwa mvumilivu kwa wanadamu,

20hata atakapoviseta viuno vyao wasio na rehema; hata atakapowalipiza kisasi mataifa;

21hata atakapouondoa utawala wa wenye kiburi, na kuzivunja fimbo za enzi za wadhalimu;

22hata atakapomlipa kila mtu sawasawa na matendo yake, na kazi za wanadamu kwa kadiri ya mawazo yao;

23hata atakapohukumu kesi ya watu wake, na kuwafurahisha kwa wokovu wake.

24Huruma huwafikia watu wakati wa mateso,

Kama mawingu ya mvua wakati wa kaskazi.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania