Hekima ya 7

Hekima ya 7

Sulemani ni sawa na watu wengine

1Mimi mwenyewe ni mwanadamu, sawa na watu wote, mzao wake aliyezaliwa kutoka mavumbini, mtu wa kwanza aliyeumbwa.

2Na ndani ya tumbo la mama yangu nikafanyizwa mwili katika muda wa miezi kumi, nikatungishwa katika damu kwa mbegu ya kibinadamu mnamo upendezi wa kitandani.

3Mimi nami nilipozaliwa, nilivuta pumzi sawa na wengine, nikaanguka juu ya nchi yenye asili moja nami, na sauti ya kwanza niliyoitoa ilikuwa kilio, kama watu wote.

4Nikalelewa, nikavikwa mavazi ya kitoto, nikatunzwa kwa uangalifu.

5Maana hakuna mfalme aliyekuwa na mwanzo mwingine;

6watu wote huingia maishani kwa njia moja, na wote hutoka kwa njia moja.

Sulemani aheshimu Hekima

7Kwa sababu hiyo niliomba, nikapewa ufahamu; nilimwita Mungu, nikajiliwa na roho ya Hekima.[#1 Fal 3:6-9; Hek 9:1-8]

8Niliichagua kuliko fimbo ya enzi na viti vya enzi, wala mali sikudhani kuwa ni kitu ikilinganishwa nayo;

9wala sikuifananisha na kito cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo mbele yake, na fedha itahesabiwa kama udongo.

10Niliipenda kupita afya njema na uzuri wa sura, hata zaidi ya nuru nikataka kuwa nayo, kwa maana mwangaza wake haufifii kamwe.

11Pamoja nayo nikajiliwa na mema yote ya jamii, na mikononi mwake mali isiyoweza kuhesabika.

12Nami nikayafurahia hayo yote, kwa sababu Hekima ni kiongozi wake; ingawa sijajua kama yeye ndiye aliyeyazaa.

13Kama mimi nilivyojifunza pasipo hila, vivyo hivyo nawashirikisha watu pasipo choyo; mimi sifichi utajiri wake.

14Maana yeye amekuwa hazina kwa wanadamu isiyowaishia; nao wale waitumiao hujipatia urafiki na Mungu, wamesifiwa mbele zake kwa ajili ya karama zinazopatikana kwa malezi.

Sulemani Aomba Kupewa Hekima

15Lakini mimi Mungu anijalie kunena kwa akili, na kuwaza mawazo mazuri yastahiliyo yale niliyokwisha kujaliwa. Kwa kuwa Yeye mwenyewe ndiye kiongozi na Hekima, naye huwarudi wao walio na hekima.

16Kwa maana tumo mikononi mwake, sisi na maneno yetu; na ufahamu wote, na ujuzi wote wa ufundi kadha wa kadha.

17Madhali Yeye mwenyewe alinipa kujua kwa sahihi mambo yaliyoko; huluka ya ulimwengu na maungamanisho ya maumbile yake;

18mianzo ya nyakati, na miisho yake, na katikati yake; zamu za vituo vya jua, na mabadiliko ya majira;

19mafuatano ya miaka na makundi ya nyota;

20asili ya viumbe hai, ukali wa hayawani, mshindo wa dhoruba, na mawazo ya binadamu; wa mimea umbalimbali na matumizi ya mizizi yake.

21Mambo yote yaliyo ya siri na yaliyo dhahiri nilijifunza; kwa kuwa Yeye aliyeyaratibisha yote pia alinifundisha, yaani Hekima.

Hali ya Hekima

22Mradi ndani yake mna roho ya welekevu, takatifu, ya pekee, yenye namna mbalimbali, iliyoerevuka, nyepesi kuenea, dhahiri kusema, safi, wazi, isiyoharibika, ya kupenda wema, hodari

23bila kuzuiwa, yenye ukarimu, ya kupenda wanadamu, thabiti, amini, bila mashaka, yenye nguvu, yenye kuangalia mambo yote, na kuingiliana na roho zote zilizo na welekevu, zilizo safi, zilizoerevuka sana.

24Kwa sababu Hekima huenda upesi kila upande hata kupita mwendo wowote, naam, huenea kotekote katika mambo yote na kupenya ndani yake kwa ajili ya usafi wake.

25Maana ndiyo pumzi ya uweza wa Mungu, na miminiko nakawa la utukufu wake Mwenyezi, hivyo lolote lililo najisi haliwezi kuingia ndani yake.

26Ndiyo mwangaza kutoka kwa nuru ya milele, na kioo kisicho na mawaa cha kutenda kwake Mungu, na mfano wa wema wake.

27Nayo ni moja, ina uwezo wa kutenda yote; hujikalia, huweza kuhuisha yote; na tangu kizazi hata kizazi huwaingilia roho takatifu, huwafanya wanadamu kuwa rafiki za Mungu na manabii;

28maana Mungu humpenda yeye tu akaaye na Hekima.

29Nzuri kuliko jua, Hekima hupita makundi ya nyota; ikilinganishwa na nuru, huonekana ya kuwa imezidi;

30mradi baada ya nuru ya mchana hufuata usiku bali juu ya Hekima hakuna ovu liishindalo.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania