Tobiti 11

Tobiti 11

Kuwasili nyumbani

1Basi, walipokaribia njia ya Kaserini, mkabala na mji wa Ninewi,

2Rafaeli akasema, “Tobia, unajua hali tuliyomwacha baba yako;

3yafaa tumtangulie mkeo, ili tukatayarishe nyumba kabla ya wengine kufika.

4Usisahau kuchukua ile nyongo ya samaki.” Basi, Tobia na Rafaeli wakatangulia nyumbani, mbwa wa Tobia akiwafuata.

5Wakati huo huo, Ana alikuwa amekaa anachungulia barabarani, akitazamia kumwona mwanawe.

6Ghafla akamwona anakuja! Ana akamwambia Tobiti kwa furaha, “Tazama! Mwanao anakuja! Anakuja na rafiki yake!”

7Kabla hawajamfikia Tobiti, Rafaeli akamwambia Tobia, “Nakuhakikishia, macho ya baba yako yatafunguliwa.

8Utaitia ile nyongo ya samaki machoni mwake, nayo dawa itanyausha vile vigamba vyeupe na baba yako ataweza kuona tena.”

9Ana akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumwambia, “Nimekuona tena mwanangu. Sasa naweza kufa!” Akatoa machozi.

Kupona kwa Tobiti

10Tobiti naye akasimama, akamwendea akijikwaakwaa akapita mlango wa ua.

11Tobia akiwa na ile nyongo ya samaki mkononi, akamkimbilia baba yake. Alimpulizia baba yake machoni na kumtegemeza. Akamwambia, “Baba, jipe moyo.”

12Kisha akamtia ile dawa machoni

13na baadaye akabandua utepe wa vigamba pembeni mwa macho yake.

14Basi, Tobiti akamkumbatia Tobia na kulia kwa furaha: “Ninakuona mwanangu! Wewe ni mwanga wa macho yangu!” Kisha akasema,

“Atukuzwe Mungu!

Litukuzwe jina lake milele!

Watukuzwe malaika wake wote watakatifu.

15Yeye aliniletea mateso haya

lakini sasa amenionea huruma,

na naweza kumwona mwanangu Tobia!”

Hapo Tobia akaingia nyumbani kwa furaha, akimsifu Mungu kwa sauti. Kisha akamwambia baba yake jinsi safari yake ilivyofanikiwa na kwamba, aliileta ile fedha, na jinsi alivyomwoa Sara, binti Ragueli, ambaye alikuwa anamfuata, karibu kufika Ninewi.

Sara awasili

16Basi, Tobiti kwa sifa za shangwe kwa Mungu alitoka kwenda kumlaki mke wa mwanawe kwenye lango la mji wa Ninewi. Watu wa Ninewi walipomwona Tobiti anatembea kwa nguvu kama zamani bila kuongozwa na mtu wakashangaa.

17Tobiti aliwaambia wote jinsi Mungu alivyomwonea huruma na kumwezesha kuona tena.

Hatimaye Tobiti akakutana na Sara mke wa mwanawe, akamkaribisha: “Karibu binti yangu! Atukuzwe Mungu aliyekuleta kwetu binti yangu. Abarikiwe baba yako! Abarikiwe mwanangu Tobia na ubarikiwe wewe binti yangu! Ingia nyumbani kwako, karibu kwa furaha na baraka, binti yangu!” Siku hiyo ilikuwa siku ya furaha kubwa kwa Wayahudi wote wa Ninewi.

18Ahika na Nadabu, binamu za Tobiti walikuja kufurahi pamoja na Tobiti.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania