Tobiti 12

Tobiti 12

Malaika Rafaeli

1Baada ya sherehe za harusi, Tobiti alimwita mwanawe Tobia, akamwambia, “Mwanangu, hakikisha kwamba unamlipa rafiki yako aliyesafiri nawe mshahara wake na kumwongezea kitu.”

2Tobia akamwuliza, “Baba, nitamlipa kiasi gani? Hata kama nikimpa nusu ya mali tuliyoleta pamoja singejali.

3Yeye amenifikisha nyumbani salama salimini; alimponya mke wangu, akaileta ile fedha pamoja nami, na sasa amekuponya wewe! Nitampa nini kwa hayo yote?”

4Tobiti akajibu, “Anastahili nusu ya yote aliyokusaidia kupata.”

5Basi, Tobia akamwita Rafaeli, akamwambia, “Chukua nusu ya mali yote uliyonisaidia kupata, kama mshahara wako. Nakutakia safari njema!”

6Lakini Rafaeli akawaita faraghani Tobiti na Tobia, akawaambia, “Mtukuzeni Mungu; tangazeni sifa zake kwa watu wote kwa ajili ya fadhili alizowafanyia. Mtukuzeni na kulisifu jina lake. Watangazieni watu wote matendo ya Mungu kama ipasavyo na wala msichoke kumshukuru.

7Yafaa kutunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu ni lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tendeni mema nanyi hamtapata madhara.

8“Afadhali sala pamoja na ukweli na kusaidia maskini pamoja na kutenda haki kuliko kuwa tajiri na kukosa uaminifu. Afadhali kusaidia maskini kuliko kulimbikiza dhahabu.

9Sadaka kwa maskini humwokoa mtu na kifo na kumtakasa dhambi zake zote. Wale wanaowasaidia maskini watajaliwa uhai,

10lakini wale wanaotenda dhambi na kufanya uovu hujiletea madhara wao wenyewe.

11“Sasa nitawajulisheni ukweli wote bila kuwaficheni chochote. Nilikwisha waambia kwamba yafaa kuitunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tobiti!

12Wewe na Sara mlipokuwa mnasali wakati ule, mimi ndiye niliyewasilisha sala zenu mbele ya Bwana aliye mtukufu. Na kila ulipokuwa unawazika wafu, mimi niliwasilisha matendo yako mbele yake.

13Wakati wewe hukusita hata kidogo kuinuka na kukiacha chakula ukaenda kumzika mtu aliyekufa, Mungu alinituma nikujaribu.

14Lakini pia alinituma kukuponya na kumwokoa mke wa mwanao, Sara.

15Mimi ni Rafaeli, mmoja wa wale malaika saba wanaokaa tayari daima mbele yake Bwana aliye mtukufu kumtumikia.”

16Tobiti na Tobia wakashikwa na hofu kubwa, wakasujudu wakiogopa sana.

17Lakini Rafaeli akawaambia, “Msiogope! Muwe na amani. Mtukuzeni Mungu milele.

18Mimi nilipokuwa kati yenu haikuwa kwa kutaka kwangu mwenyewe, bali kwa kutaka kwake Mungu. Yeye ndiye mnayepaswa kumtukuza maisha yenu yote. Yeye ndiye mnayepaswa kumsifu.

19Nyinyi mlidhani mliniona nikila chakula, lakini ni kwa kuonekana tu na haikuwa hivyo.

20Basi, sasa mtukuzeni Bwana duniani na kumshukuru. Mimi narudi sasa kwake yeye aliyenituma kutoka juu. Andikeni mambo hayo yote yaliyotukia.”

21Kisha Rafaeli akatoweka, wasimwone tena.

22Basi wakamsifu Mungu kwa nyimbo, wakamshukuru kwa ajili ya matendo yake makuu aliyowafanyia malaika wake Mungu alipokuwa amewatokea.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania