Hekima ya Solomoni 16

Hekima ya Solomoni 16

Mapigo ya Wamisri

1Kwa hiyo, watu hao waliadhibiwa kwa viumbe hivyohivyo kama walivyostahili;

naam, waliteswa kwa makundi ya viumbe hao.

2Lakini wewe, ee Bwana, badala ya kuwaadhibu hivyo watu wako, uliwahurumia.

Uliwaweka kware tayari kwa chakula,

chakula cha kigeni na kitamu, kuridhisha hamu yao.

3Ulifanya hivyo kusudi watu wale walioabudu miungu,

wakiona njaa wapoteze hata ladha ya kula

kwa sababu ya viumbe vile vya kuchukiza walivyopelekewa.

Lakini watu wako walipata njaa kwa muda mfupi,

kisha wakapata chakula kile kitamu sana.

4Iliwapasa wale wadhalimu wa watu wako kuteseka kwa kupungukiwa mahitaji,

hali watu wako walishuhudia jinsi maadui zao walivyoteswa.

5Watu wako walipokabiliwa na wanyama wa kutisha

na nyoka wenye sumu kuwaua baadhi yao,

wewe hukuendelea kwa muda mrefu kukasirika mpaka mwisho.

6Walisumbuliwa kwa muda mfupi tu kama onyo kwao.

Kisha ukawapa ile ishara ya kuwaponya,

ili uwakumbushe matakwa ya sheria yako.

7Kama mtu akiitazama alama hiyo aliponywa,

lakini kilichomponya sio hicho kitu alichokiona,

bali wewe uliye Mwokozi wa watu wote.

8Naam, kwa kufanya hivyo uliwahakikishia maadui zetu

kwamba wewe ndiwe unayewaokoa watu katika baya lolote.

9Maadui zetu waliuawa kwa kuumwa na nzige na nzi,

wala haikuwako njia yoyote ya kuwaponya,

kwa sababu walistahili kuadhibiwa kwa viumbe hivyo.

10Lakini hata nyoka wenye sumu hawakuweza kuwaangamiza watu wako,

maana wewe ulikuja kwa huruma yako ukawaponya.

11Waliumwa na nyoka wapate kuyakumbuka maagizo yako,

lakini waliokolewa upesi,

wasije wakakusahau kabisa,

na kuwa wazembe kuhusu wema wako.

12Waliponywa sio kwa mitishamba, wala kwa dawa yoyote ile,

bali kwa neno lako, ee Bwana, lenye kuwaponya watu wote.

13Wewe unao uwezo juu ya uhai na kifo;

waweza kuwaporomosha watu mpaka kuzimu na kuwarudisha tena.

14Mtu mbaya aweza kumwua mwingine,

lakini hawezi kumrudishia uhai huyo aliyekufa,

wala kuiokoa roho iliyofungwa huko kuzimu.

Balaa lililowapata Wamisri

15Hakuna mtu awezaye kukutoroka wewe.

16Wale watu waovu walikataa kukutambua wewe,

ukawaadhibu kwa nguvu za mkono wako.

Walikabiliwa na dhoruba kali, mvua ya mawe na tufani zisizokoma,

wakateketezwa kabisa kwa moto.

17Ajabu ni kwamba katika maji ambayo kawaida huzima moto,

moto huo uliwaka kwa nguvu zaidi

maana nguvu zote za maumbile huwalinda waadilifu.

18Wakati mmoja, moto huo huo ulipungua nguvu yake

ili usije ukaangamiza vile viumbe vilivyopelekwa kuwaadhibu waovu

ili watu hao waone na kutambua kwamba waliandamwa na hukumu yako.

19Tena, mara nyingine moto huo uliwaka kwa ukali zaidi ya moto katika maji,

ukateketeza mazao ya nchi walimoishi hao waovu.

Watu wa Israeli wanapewa mana

20Lakini badala ya balaa hilo uliwapa watu wako chakula cha malaika;

uliwashushia mkate tayari kwa kula toka mbinguni, bila ya jasho lao,

mkate uliowafurahisha kwa kila namna na kutosheleza ladha ya kila mtu.

21Chakula chako kilidhihirisha unavyowaangalia kwa upendo watoto wako.

Chakula hicho kilishibisha tamaa ya kila mtu aliyekila;

tena kilijichanganya chenyewe na kumfaa kila mmoja kadiri alivyotaka.

22Chakula chenyewe ingawa kilifanana na theluji au barafu,

hakikuyeyushwa na ule moto;

hiyo iliwafundisha watu wako kwamba ule moto ulioangamiza mazao ya maadui zao

wakati wa tufani na mvua ya mawe,

23ulijiachilia nguvu yake ili watu wako waadilifu wapate chakula.

24Ulimwengu uliouumba uko chini ya amri yako,

na hutumia nguvu yake kuwaadhibu watu waovu;

lakini hupungua nguvu yake ili kuwafaa wanaokutegemea.

25Kwa hiyo, wakati ule, ulimwengu ulijirekebisha namna kwa namna,

kuonesha jinsi unavyohifadhi kwa ukarimu mahitaji ya wote wanaokuomba.

26Ilifanyika hivyo ili watoto wako uwapendao, ee Bwana,

wajifunze kwamba hatulishwi kwa mazao tunayolima,

bali neno lako ndilo linalowahifadhi wale wanaokutumainia.

27Chakula kile ambacho hakikuharibiwa katika ule moto,

kiliyeyuka asubuhi kilipopata joto hafifu la jua.

28Na hiyo ilitufundisha kwamba tunapaswa kuamka kabla ya pambazuko kutoa shukrani zetu kwako

na kusali wakati jua linapochomoza.

29Maana tumaini la mtu asiye na shukrani huyeyuka kama umande,

hutoweka kama maji yasiyo na faida.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania